Mikopo kwa Vituo vya Matibabu

Utangulizi

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ukiwa na azma ya msingi ya kuboresha huduma za matibabu kwa wanachama wake na watanzania kwa ujumla, unatoa mikopo yenye riba nafuu ya vifaa tiba, dawa na ukarabati wa majengo kwa watoa huduma za matibabu waliosajiliwa na Mfuko ili waweze kukarabati na kuboresha majengo ya kutolea huduma za matibabu, kununua dawa na vifaa tiba.

Vigezo na Mambo ya Msingi ya Kuzingatia

Mikopo ipo wazi kwa mtoa huduma yeyote aliyesajiliwa na Mfuko kwa kuzingatia yafuatayo:-

 • Uwezo wa kituo kurejesha mkopo kwa wakati uliopangwa;
 • Marejesho ya mkopo yatafanywa kwa njia ya makato kutoka kwenye madai ya kila mwezi ya kituo yanayowasilishwa kwenye Mfuko;
 • Kituo kinatoa huduma kwa kuzingatia kanuni na miongozo ya matibabu nchini;
 • Mikopo inayotolewa ni ya vifaa tiba, dawa na ukarabati wa majengo na sio fedha taslimu; na
 • Muda wa marejesho ya mkopo ni kati ya miezi 12 hadi miezi 60 kulingana na aina ya mkopo na ukubwa wa mradi.

Taratibu za Utoaji Mikopo

Taratibu za Ujumla

 • Mwombaji atahitajika kuandika barua ya maombi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko; na
 • Mwombaji atahitajika pia kujaza fomu ya maombi ya mkopo (NHIF/7) inayopatikana katika ofisi zote za Mfuko na tovuti ya Mfuko. Ada ya fomu ni Sh. 20,000/- inayolipwa wakati wa kurejesha fomu;

Taratibu kwa Aina ya Mkopo

Mkopo wa Vifaa Tiba na Dawa

 • Mwombaji anapaswa kuomba kifaa tiba au dawa inayoruhusiwa kutumika katika ngazi ya kituo husika kulingana na Mwongozo wa Matibabu nchini;
 • Ombi la mkopo likikubaliwa, mwombaji atatakiwa kuendelea na taratibu za manunuzi na kuwasilisha kwa Mfuko nyaraka husika (Contracts & proforma invoices) za mzabuni/msambazaji aliyeteuliwa na mwombaji;
 • Mfuko utaingia mkataba wa mkopo na mwombaji;
 • Mfuko utatoa idhini ya mzabuni kusambaza vifaa tiba au dawa husika kwa mwombaji baada ya mkataba wa mkopo kusainiwa (kwa taasisi za umma msambazaji wa kwanza atakuwa Ghala la Taifa la Dawa);
 • Mwombaji atatakiwa kutoa taarifa ya kuridhika au kutoridhika na kifaa kwa kujaza fomu maalum na kuiwasilisha katika ofisi ya Mfuko; na
 • Mfuko utamlipa mzabuni baada ya kukaguzi wa vifaa tiba au dawa husika.

Mkopo wa Ukarabati Majengo

 • Ombi la ukarabati majengo likikubaliwa, mwombaji atatakiwa kuwasilisha au kuingia mkataba na mkandarasi pamoja na mshauri/msimamizi wa mradi;
 • Mwombaji atatakiwa vilevile kuambatanisha/kuwasilisha michoro ya ujenzi (construction drawings) na makadirio ya ujenzi (Bills of Quantities);
 • Mfuko utaingia mkataba wa mkopo na mwombaji na kuruhusiwa kuendelea na ujenzi;
 • Malipo ya ujenzi (payment certificates) yatafanywa moja kwa moja kwa Mkandarasi yakiwa yameidhinishwa na mshauri/msimamizi wa mradi. Mfuko utakagua mradi kabla ya malipo husika kufanyika; na
 • Utekelezaji wa mradi kwa utaratibu wa “force account” kwa taasisi za umma utazingatiwa.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na ofisi ya NHIF iliyo karibu nawe piga simu bila malipo 0800110063.