MAKAMU WA RAIS AIELEKEZA NHIF KUWAFIKIA WANANCHI VIJIJINI

Imewekwa: 12 July, 2025
MAKAMU WA RAIS AIELEKEZA NHIF KUWAFIKIA WANANCHI VIJIJINI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philipo Mpango ameuelekeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuweka mikakati ya kuwafikia wananchi walioko vijijini ili waweze kunufaika na huduma za matibabu kupitia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya.

Agizo hilo amelitoa leo wakati akitembelea mabanda kwenye  Mkutano Mkuu wa Waganga Wakuu wa Wilaya unaoendeleq Jijini Dodoma.

“Ninaelekeza Mfuko kufika vijijini waliko wananchi wengi na kuwasajili ili waweze kuwa na uhakika wa huduma za matibabu, wekeni mkakati katika suala hili,” alielekeza.

Katika hatua nyingine Mhe. Dkt. Mpango amepongeza jitihada zinazochukuliwa na Mfuko katika kupanua wigo wa huduma ambapo amesisitiza ushirikiano kati ya NHIF, Wizara ya Afya na TAMISEMI katika kujenga uelewa wa wananchi katika suala la  bima ya afya ili kufikia lengo la serikali la kila mtanzania kuwa na uhakika wa matibabu wakati wote.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama akitoa ufafanuzi wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote inavyouwezesha Mfuko kujipambanua katika usajili wa wanachama katika makundi mbalimbali mbele ya makamu wa Rais Dkt. Philipo Mpango alipotembelea Banda wa NHIF katika Mkutano wa waganga wakuu wa Halmashauri na Mikoa unaoendelea jijini Dodoma.

Kwa upande wa Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa kutokana na maboresho ya sheria, kanuni na taratibu zinaiwezesha Mfuko kwa sasa kufikia makundi yote ya wananchi.

“Katika hili la Bima ya Afya kwa Wote, NHIF ni mdau mkubwa sana hivyo ni matarajio yetu atawafikia wananchi wengi zaidi na kuwapa huduma bora” alisema Mhe. Waziri.

Akitoa maelezo ya awali, Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu Dkt. David Mwenesano alisema kuwa kwa sasa Mfuko unaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa bima ya afya kwa wote ikiwemo kutoa elimu, kuimarisha mifumo ya usajili na ulipaji wa madai ili kuweza kuhudumia wananchi wengi zaidi.

BIMA YA AFYA KWA WOTE, JIUNGE SASA