KfW yaipongeza NHiF kwa kuanza utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote

Imewekwa: 13 July, 2025
KfW yaipongeza NHiF kwa kuanza utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote

Na Mwandishi Wetu Dodoma,

Menejimenti ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Irene C. Isaka imefanya mazungumzo na Uongozi wa Wadau wa Maendeleo, Benki ya Kreditanstalt fùr Wiederaufbau (KfW). KfW ni Benki ya Serikali ya Ujerumani inayohusika na masuala ya Maendeleo na Uwekezaji.

Mara baada ya Dkt. Isaka kutoa maelezo ya utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote,
 Mkurugenzi wa KfW anayesimamia Afrika Mashariki pamoja na Umoja wa Afrika Bw. Christoph Tiskens, aliipongeza NHiF kwa kuanza utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kwa makundi Maalum. Alisema hili ni jambo kubwa ambalo litabadili kabisa huduma za afya kwa wananchi na kuleta maendeleo ya kiafya na kiuchumi.

Katika mazungumzo hayo Bw. Tiskens alisema anatambua gharama kubwa za bima ya afya kwa kaya maskini pamoja na magonjwa yasiyoambukiza, alisema KfW itashiriki kusaidia Mfuko wa kusaidia ndoto ya Bima ya Afya kwa Wote kutimia kupitia Benki ya Dunia.

Majadiliano hayo yaliangazia ushirikiano unaoendelea kati ya Mfuko na KfW kupitia mradi wa maboresho ya mifumo ya TEHAMA  pamoja na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.

 Katika kikao hicho, KfW ilitumia fursa hiyo kumtambulisha Mtendaji Mkuu mpya wa taasisi hiyo kwa Tanzania, Ms. Vanessa Eidt akichukua nafasi ya Mtendaji Mkuu anayemaliza muda wake  Ms. Jennifer Worl.

Katika kuhitimisha kikao hicho, pande zote mbili ziliahidi kuendeleza ushirikiano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

"Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa"