Mikopo ya Vifaa Tiba na Ukarabati wa Majengo

MIKOPO YA VIFAA TIBA, UKARABATI WA MAJENGO NA DAWA KWA VITUO VYA

KUTOLEA HUDUMA ZA MATIBABU

Utangulizi

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) una jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama wake. Na katika kutekeleza hilo Mfuko unatoa mikopo ya vifaa tiba, ukarabati wa majengo na dawa kwa watoa huduma za matibabu waliosajiliwa na Mfuko yenye riba nafuu.

Vigezo na Mambo ya Msingi ya Kuzingatia

Mikopo inatolewa kwa watoa huduma wote waliosajiliwa na Mfuko kwa kuzingatia yafuatayo:-

 • Uwezo wa kituo kurejesha mkopo kwa wakati uliopangwa;
 • Mikopo inayotolewa ni ya vifaa tiba, dawa na ukarabati wa majengo na sio fedha taslimu.
 • Marejesho ya mkopo yatafanywa kwa kupitia makato kutoka kwenye madai ya kila mwezi ya kituo yanayowasilishwa kwenye Mfuko;
 • Muda wa marejesho ya mkopo ni kati ya miezi 12 hadi miezi 60 kulingana na aina ya mkopo na ukubwa wa mradi.

Taratibu za Utoaji Mikopo

Taratibu za Ujumla

 • Mwombaji atahitajika kuandika barua ya maombi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko na kuiwasilisha ktika ofisi ya NHIF iliyo karibu;
 • Mwombaji atahitajika kujaza fomu ya maombi ya mkopo (NHIF/7) inayopatikana katika ofisi zote za Mfuko na tovuti yake.
 • Mwombaji atalipia ada ya fomu Sh. 20,000/- inayolipwa wakati wa kurejesha fomu;

Taratibu za Mkopo ya Vifaa Tiba na Dawa

 • Mwombaji anapaswa kuomba kifaa tiba au dawa inayoruhusiwa kutumika katika ngazi ya kituo husika kulingana na Mwongozo wa Matibabu nchini;
 • Ombi la mkopo likikubaliwa, mwombaji atatakiwa kuendelea na taratibu za manunuzi na kuwasilisha kwa Mfuko nyaraka husika mikataba na ankara ya malipo ya mzabuni/ msambazaji aliyeteuliwa na mwombaji.
 • Mfuko utaingia mkataba wa mkopo na mwombaji/ kituo husika.
 • Mfuko utatoa idhini ya mzabuni kusambaza vifaa tiba au dawa husika kwa mwombaji baada ya mkataba wa mkopo kusainiwa.
 • Mwombaji atatakiwa kutoa taarifa ya kuridhika au kutoridhika na kifaa kwa kujaza fomu maalum na kuiwasilisha katika ofisi ya Mfuko.
 • Mfuko utamlipa mzabuni baada ya ukaguzi wa vifaa tiba au dawa katika kituo husika.

Taratibu za Mikopo ya Ukarabati

 • Ombi la ukarabati majengo likikubaliwa, mwombaji atatakiwa kuwasilisha au kuingia mkataba na mkandarasi pamoja na mshauri/msimamizi wa mradi;
 • Mwombaji atatakiwa kuambatanisha/ kuwasilisha michoro ya ujezi na makadirio ya ujenzi (Bills of Quantities).
 • Mfuko utaingia mkataba na mwombaji/ kituo na kuruhusiwa kuendelea na ujenzi
 • Mfuko utakagua mradi kabla ya malipo ya ujenzi (payment certificates) na malipo hayo yatafanywa moja kwa moja kwa mkandarasi yakiwa yameidhinishwa na mshauri/ msimamizi wa mradi.

Utekelezaji wa mradi kwa utaratibu wa “force account” kwa taasisi za umma utazingatiwa.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na ofisi ya NHIF iliyo karibu nawe piga simu bila malipo 199.