TUMEIDHINISHA KITITA CHA NHIF- MHE. UMMY

TUMEIDHINISHA KITITA CHA NHIF- MHE. UMMY May 13, 2024

SERIKALI imeidhinisha matumizi ya kitita kipya cha mafao cha Mfuko wa Taifa waBima ya Afya cha mwaka 2023 ambacho kimeoanishwa na Orodha Muhimu ya Dawa (NEMLIT) pamoja na Mwongozo wa Tiba wa Taifa (STG).

Akiwasilisha hotuba ya Makadilio ya bajeti, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Kikita hicho kitaboresha upatikanaji wa huduma bora za kibingwa na ubingwa bobezi karibu na wanachama.

Alisema kuwa kitita hichoi kimezingatia maendeleo ya teknolojia ya tiba, hali halisi ya bei katika soko na uwezo wa Mfuko kugharamia huduma hizo huku ukiendelea kuwa endelevu kwa kuzingatia ushauri wa Taarifa ya mapendekezo ya Tathmini ya Uhai na uendelevu kwa kipindi kinachoishia Juni 30, 2021.

“Mheshimiwa Spika, Mambo makubwa yaliyofanyiwa maboresho katika kitita cha mafao cha mwaka 2023 ni pamoja na kuongeza dawa mpya 254 zenye ufanisi ambazo awali wanachama walilazimika kutoa fedha taslimu kwakuwa hazikuwa sehemu ya Kitita cha mwaka 2016, kuongeza Dawa 178 ambazo hazikuwa kwenye Orodha ya Dawa Muhimu ya Taifa (NEMLIT) baada ya Wizara kufanya mapitio ya NEMLIT na kutoa nyongeza (addendum) na hivyo kujumuishwa katika kitita cha NHIF cha mwaka 2023,” alifafanua Mhe. Ummy.

Ameeleza kuwa manufaa makubwa ya maboresho ya kitita hicho ni pamoja na kuwaepusha wanachama kuendelea kutumia dawa zisizo na matokeo chanya hivyo kuondoa uwezekano wa wagonjwa kupata magonjwa yasiyoambukizwa kutokana na usugu wa dawa husika.

Mhe. Ummy ameweka wazi kuwa Kitita hicho kinasogeza huduma za kibingwa na ubingwa bobezi karibu na wananchi kuanzia Hospitali za ngazi mkoa na Kanda hivyo kuondoa usumbufu wa kukosa baadhi ya dawa na huduma nyingine. Amezitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na matibabu ya saratani, upasuaji wa mifupa, upasuaji wa moyo ambazo awali zilikuwa zinatolewa katika Hospitali za ngazi ya Taifa tu.

Kutokana na haya, alisema kwa kutambua huduma za afya zinabadilika mara kwa mara na kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia na hali halisi ya soko, ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza na kukua kwa Sekta ya Afya ya umma na binafsi, NHIF itafanya mapitio ya kitita cha mafao yake kila baada ya miaka miwili (2).

Aidha, Serikali inakusudia kuanzisha Chombo cha Kitaifa cha Udhibiti wa Bei za Huduma za Afya katika ngazi zote nchini kama inavyofanyika kwenye udhibiti wa gharama za maji, umeme na mafuta. Lengo ni kudhibiti ukuaji holela wa gharama za afya kwa wananchi hususan wasio na bima ya afya.