Kusainiwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kunaleta matumaini makubwa kwa wananchi kwa kuwa utekelezaji wake utawezesha wananchi wote kupata huduma za matibabu bila vikwazo.
Sheria hii tayari imeshasainiwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Tanzania Novemba mwaka huu na sasa inasubiriwa kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali kwa ajili ya kuanza utekelezaji wake.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, kila mwananchi atakuwa na uhuru wa kuchagua skimu ya bima ya afya na kujiunga nayo ili kumwezesha kupata huduma za matibabu wakati wowote anapohitaji.
Sheria hiyo inaweka Mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote ambapo makundi mbalimbali yatajumuishwa ikiwa ni pamoja na Watumishi wa Umma na wa sekta binafsi, waliojiajiri wenyewe katika sekta isiyo rasmi na wananchi wasio na uwezo ambao sheria imeweka utaratibu wa kuwawezesha kuwa na bima ya afya.
Kuwepo kwa Sheria hii kuna faida ambazo hazikuweza kupatikana awali kutokana na kuwepo na wachache waliojiunga na kunufaika na hivyo kufanya kuwepo kwa kundi kubwa wasio nufaika. Sheria hii itawezesha uhakika wa matibu kwa wote; kuimarisha uboreshaji wa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya vya Umma na binafsi, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa upatikanaji wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba.
Manufaa mengine ni kuimarika kwa uhimilivu na ustahimilivu wa Skimu za bima ya afya kutoa huduma kwa kuwa wananchi watapaswa kuchangia kabla ya kuugua katika Skimu za Bima ya Afya.
Serikali imeshawekeza kwenye miundombinu ya afya. Lililobaki ni wananchi sasa kuwa na uwezo wa kukuzipata huduma hizo na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ndio suluhisho.