NHIF WALA KIAPO CHA KUWATUMIKIA WATANZANIA KWA UADILIFU

NHIF WALA KIAPO CHA KUWATUMIKIA WATANZANIA KWA UADILIFU Oct 14, 2024

Jumla ya watumishi 410 wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wamekula kiapo cha kutunza siri na kuwatumikia Watanzania kwa weledi na kwa kufuata maadili ya Utumishi wa Umma.

Zoezi hili limefanyika siku ya Jumamosi Tarehe 12 Oktoba na Jumapili Tarehe 13 Oktoba,2024 Jijini Dodoma wakati wa Mafunzo Elekezi kwa Maofisa Udhibiti Ubora, Maofisa Madai na Maofisa Wanachama.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka amesema kuwa umuhimu wa mafunzo hayo na kiapo ni kuwakumbusha Watumishi wa Mfuko kuwa wana wajibika kwa Wanachama, Wadau wa Mfuko na wananchi kwa ujumla.

Aliwakumbusha dhamana kubwa waliyopewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo wanatakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni, miongozo ya Sera, Sheria, kanuni na taratibu na kutekeleza majikumu yao kwa uadilifu mkubwa.

Aliwakumbusha kwamba tuache kufanya kazi kwa mazoea tunapowapa huduma wanachama wetu na wadau mbalimbali. Alihimiza kuwa wabunifu na kutumia mifumo ili kutatua changamoto zinazokabili Mfuko na Sekta kwa ujumla hususani katika kipindi hiki ambacho tunaanza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote.

“Ni jukumu letu sisi kuhakikisha tunawahudumia wanachama na wadau kwa weledi mkubwa na kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma na ndio maana tunakula kiapo hiki kinachotutaka pia kutunza siri za Serikali," amesema Dkt. Isaka.

Alitumia fursa hiyo kuwahimiza watumishi kuweka nguvu kubwa katika uelimishaji umma kuhusu huduma zinazotolewa na Mfuko ili kujenga uelewa kwa wadau na Umma kwa ujumla.

Katika kikao kazi hicho. Kundi la Afisa uanachama walielekezwa namna ya kutumia Mfumo wa uandikishaji wanachama, kupokea michango pamoja na namna ambayo wanachama na wadau wanavyoweza kutuma malalamiko yao kidigitali. Watumishi hao walipata mafunzo ya namna ya kutambua viashiria vya udanganyifu kwa wanachama na waajiri na hatua stahiki za kuchukua

Kwa upande mwingine kundi la Maafisa ubora na Maafisa Madai walielekezwa namna ya kutumia Mfumo wa kuchakata madai ili kulipa kwa wakati. Vile vile walipata mafunzo ya namna ya kutambua viashiria vya udanganyifu kwa watoa huduma na hatua stahiki.

Bima ya Afya kwa Wote, jiunge sasa