11 Machi 2026
Simulizi ya mabadiliko.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeshiriki kwenye zoezi la utunzaji wa mazingira jijini Arusha kwa kupanda miti maeneo mbalimbali Jijini humo. Zoezi hilo lililoongozwa na Mkurugenzi mkuu wa Mfuko Dkt. Irene C. Isaka ambapo watumishi wa Mfuko toka mikoa mbalimbali walishiriki zoezi hilo.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa zoezi hilo, Mkurugenzi Mkuu alisema; Mfuko wa NHIF unatambua umuhimu wa kulinda mazingira na pia unazingatia matakwa ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) ambapo malengo namba 13 na 15 yanasisitiza umuhimu wa kutunza mazingira ili kuokoa sayari ya dunia dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi kwa ajili ya maisha ya sasa na vizazi vijavyo. Aidha Dkt. Isaka alisema jitihada hizi zinazingatia maono ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa kinara kwenye eneo la utunzaji mazingira hasa jitihada zake kwenye hamasa ya matumizi ya nishati safi kote nchini, ikiwa ni mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, kama ilivyoelezwa kwenye Dira ya Maendeleo 2050.
Zoezi hilo ni mwendelezo wa zoezi lililofanyika mkoani Dodoma wakati wa maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2026, ambapo watumishi wanawake walipanda miti maeneo mbalimbali mkoani Dodoma.
Akizungumza na watumishi wakati wa matukio hayo, Dkt. Isaka alisema NHIF imedhamiria kwa dhati kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii kwenye eneo la utunzaji wa mazingira, Dkt Isaka aliendelea kusema duniani kote mabadiliko huja kwa wachache kuanza. NHIF tunaonesha njia tukiwa na hamasa kubwa kwamba jamii nzima itaunga mkono zoezi hili ili hatimaye nchi yetu ifikie dhamira ya malengo ya maendeleo endelevu.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Dkt.Irene Charles Isaka akizungumza na watumishi wanaume wa Mfuko baada ya zoezi la kupanda miti katika hospitali ya Jiji iliyopo Njiro Arusha.
Upandaji wa miti katika mikoa ya Dodoma na Arusha ni mwanzo tu, NHIF itaendelea na zoezi hili mikoa yote nchini kwakuwa Mfuko una ofisi na watumishi kila mkoa.
Kwa upande wa mkoa wa Arusha Mfuko umepanda jumla ya miti 1000 katika maeneo ya Hospitali ya jiji iliyopo Njiro, Kituo cha Afya Moshono, Mwivano na Olomotii.
Akihitimisha simulizi ya mabadiliko inayoandikwa na NHIF, Mkurugenzi mkuu Dkt. Isaka alishukuru Mamlaka mbalimbali kwa ushirikiano wanaotoa kwa Mfuko kufanikisha zoezi hili pamoja na wadau mbalimbali kwa jinsi wanavyopokea zoezi hili kwa mtazamo chanya.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi ya Hospiatli ya Jiji iliyopo Njiro jijini Arusha Dkt. Said Salim alishukuru uongozi wa NHIF kwa kuchagua hospitali hiyo na kupanda miti, jambo litakaloboresha mazingira ya hospitali hiyo. Tunajiona wenye bahati kufikiwa na zoezi hili, alisema Dkt. Salim.
“NHIF tutaendelea kuwa chachu ya mabadiliko katika utunzanji wa mazingira kote nchini”.

Watumishi wanaume wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wakiwa katika zoezi la upandaji wa miti Mkoani Arusha.