NHIF IMEBORESHA KITITA KUZINGATIA MIONGOZO - Makamu wa Rais

NHIF IMEBORESHA  KITITA KUZINGATIA MIONGOZO - Makamu wa Rais May 02, 2024

SERIKALI imesema kuwa maboresho yaliyofanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwenye Kitita chake cha mafao yamezingatia miongozo na orodha ya dawa muhimu za Taifa.

Hayo yamesemwa leo na Makamu wa Rais Mhe. Isdori Mpango wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Kitaifa yaliyofanyika mkoani Arusha.

"Kuhusu hoja ya Kitita cha NHIF kilichofanyiwa maboresho hivi karibuni, Mfuko umefanya hivyo ili kwenda sambamba na Maboresho yaliyofanywa na Serikali kwenye orodha ya Taifa Dawa Muhimu na miongozo ya tiba. Aidha NHIF ilikutana na TUCTA Aprili 25, 2024 na kutoa ufafanuzi wa kitita hicho," alisema Mhe. Mpango.

Kuhusu hoja ya kutoshirikishwa kwa wadau, alisema kuwa Serikali iliunda Kamati Huru kwa ajili ya kupitia hoja mbalimbali zilizoibuka na kuhakikisha kuwa wadau wote wanashirikishwa.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mpango alisema kuwa Uhai na uendelevu wa Mfuko unategemea uwasilishwaji wa michango ya wanachama wake kwa wakati, ambapo amewaelekeza waajiri wote kuwasilisha michango ya bima ya afya kwa wakati. Kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko Sura 395 mwajiri anapaswa kuwasilisha mchango ndani ya siku 30 baada ya kulipa mshahara.

Kitita kipya cha mafao cha mwaka 2023 kilianza kutumika rasmi mwezi Machi 2024 huku Kamati Huru ikiendelea kukutana na wadau wote kwa lengo la kupokea maoni na kuona namna bora ya kufanya maboresho zaidi.

Maboresho yaliyofanyika tangu kuanza utekelezaji wa kitita hicho ni pamoja na kuongeza dawa 254 ambazo awali hazikuwepo kwenye kitita cha mwaka 2016.

Mfuko unaendelea na maboresho mbalimbali ya huduma ili kuhakikisha wanachama wanapata huduma bora.