Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Uongozi wa Soko la Kisasa la Machinga lilipo Jijini Dodoma umesema uko tayari kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kuwaelimisha, kuwahamasisha na kuwasajili machinga waliopo sokoni hapo ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wote.
Soko hilo lenye zaidi ya Machinga 3,500 na linalohudumia Watanzania zaidi ya 15,000 kwa siku ni soko muhimu kwa mahitaji ya wananchi na linasaidia kuboresha na kutoa huduma kwa wananchi.
Ili kuwahakikishia usalama wa afya za machinga hao, leo NHIF ilitembelea soko hilo na kupata firsa ya kuzungumza na uongozi wa soko hilo kupitia Meneja wa Soko CPA John Kahungu ambaye alipongeza hatua ya Mfuko kufika hapo kwa lengo la kuelimisha na kujenga mahusiano.
“ Kwa hili mlilolifanya leo la kuja hapa sokoni na kukutana na machinga walioko hapa kwa kuwapa elimu na kuwahamaisha kujiunga na bima ya afya hakika ni jema sana na kwa kufanya hivi mtaamsha ari ya wafanyabiashara hawa kuona umuhimu wa bima ya afya na kujiunga,” alisema CPA Kahungu.
Watumishi wa Mfuko wa Tifa wa Bima ya Afya wakiwa katika Picha ya Pmoja na Meneja wa Soko la Machinga Complex lililopo jijini Dodoma wakati walipofika sokoni hapo kwa ajili ya kutoa elimu ya umuhimu wa Bima afya kwa wafanyabiashara wa soko hilo.
Aidha aliomba Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kupiga kambi katika soko hilo kwa ajili ya kutoa elimu na usajili wa wanachama ili wawe na uhakika na afya zao na kupanga mipango bora ya kibiashara.
Kwa upande wao Machinga waliopata fursa ya kuzungumza na timu ya tuambie tuboreshe, walifurahia hatua hiyo na kusema wako tayari kujiunga na huduma za NHIF kwa kuwa wamepata elimu na kujua manufaa ya bima ya afya.
Mfuko unaendelea na kampeni yake ya kuwafikia wananchi katika maeneo yao ili kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wake. Aidha kampeni hii inalenga kupata mrejesho wa huduma ili kuboresha zaidi.
Bima ya afya kwa Wote, Jiunge sasa