Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Dkt. Irene C. Isaka leo tarehe 15 Agosti, 2025 amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa maendeleo toka Korea Kusini kwa lengo la kuangazia mashirikiano kati ya Mfuko katika eneo la kuwajengea uwezo watumishi namna bora ya utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa wote.
Akizungumza katika majadiliano hayo kiongozi wa msafara kutoka shirika la Korea Foundation for International Healthcare (KOFHI) Prof: Soonman Know alisema tayari walishaingia makubaliano na Wizara ya Afya na watakuwa na mpango kazi wa kutoa elimu kwa miezi miwili kwa wataalam ambao watajengewa uwezo kuhusu mbinu mbalimbali za utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Prof. Know amesema kuwa shirika la KOFHI limefanya mafunzo kwenye nchi za Ghana, Ethiopia na Kambodia ambapo wamefanikiwa sana katika utekelezaji wa bima ya Afya kwa Wote.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Isaka ameahidi ushirikiano wa Mfuko kwa kuhakikisha watumishi wa Mfuko kutoka idara na vitengo mbalimbali kushiriki katika mafunzo hayo ili kuweza kuongeza ujuzi katika maeneo kama uchakataji wa madai, takwimu, utafiti na tathmini ya uhai na uendelevu wa Mfuko.
Dkt. Isaka alimaliza kwa kuwashukuru sana Wadau hao muhimu kuelekea utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambapo NHIF ni mshiriki muhimu katika kufanikisha adhma ya kuwafikia Watanzania wote.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge sasa