USHIRIKA AFYA (Cooperative Health)

Ushirika Afya ni mpango mahsusi ulioanzishwa na Mfuko kwa wanachama wa vyama vya msingi vya ushirika wa mazao (kwa kuanza na mazao matano ya kimkakati ambayo ni Pamba, Kahawa, Chai, Korosho na Tumbaku). Utaratibu huu unatoa fursa kwa mkulima kusajiliwa katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kupitia chama chake cha msingi cha ushirika wa mazao.

Mwanachama wa Ushirika Afya atachangia Shilingi 76,800 kwa mwaka na atapatiwa kadi ya matibabu ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambayo ataitumia kupata matibabu katika vituo zaidi ya 7000 vilivyosajiliwa na Mfuko

nchi nzima. Aidha, kupitia utaratibu huu mkulima ana fursa ya kumwandikisha mwenza wake, mzazi au mzazi wa mweza kwa kuongeza malipo ya TZS 76,800 kwa kila mmoja kwa mwaka. Endapo mwanachama wa Ushirika Afya atahitaji kuwasajili watoto katika mpango huu atalipa TZS 50,400 kwa mwaka kwa kila mtoto chini ya miaka 18

MAFAO YATOLEWAYO

Mwanachama wa NHIF katika utaratibu wa Ushirika Afya apata mafao yote yanayotolewa na Mfuko sawa sawa na wanachama wengine chini ya Mfuko huu wanaojiunga kwa taratibu nyingine. Mafao hayo yanahusisha gharama za:-

• Kujiandikisha na Kumwona daktari

• Dawa zote muhimu zilizoidhinishwa na Serikali

• Vipimo vidogo na vikubwa

• Kulazwa

• Upasuaji mdogo, mkubwa pamoja na upasuaji wa kujifungua kwa wanawake

• Matibabu ya kinywa na meno

• Matibabu ya macho pamoja na miwani ya kusomea

• Mazoezi ya kimatibabu ya viungo (physiotherapy)

• Vifaa saidizi kama magongo, vishikizi vya shingo

Pia mwanachama atatumia kadi yake katika vituo zaidi ya 7,000 nchi nzima kuanzia zahanati hadi Hospitali za rufaa za serikali, binafsi na hata za madhehebu ya dini pamoja na maduka ya dawa yaliyosajiliwa na NHIF.

JINSI YA KUJISAJILI

Ili kujisajili, chama chenye sifa zilizotajwa hapo juu kitajaza fomu maalum ya taarifa maalumu za chama na kuingia makubaliano na Mfuko. Mwanachama wa chama cha Ushirika atajaza fomu maalumu ya taarifa zake na kujisajili na Mfuko. Chama kitakuwa na wajibu wa kukusanya michango ya wanachama wake wanaojisajili na NHIF na kuiwasilisha katika Mfuko. Mwanachama atapatiwa kadi ya matibabu ya Mfuko ambayo ataitumia kupata huduma za matibabu katika vituo vilivyosajiliwa na Mfuko Tanzania Bara na Visiwani.