Boda boda Afya

Bodaboda Afya ni nini?

Ni utaratibu wa bima ya afya unaowalenga waendesha bodaboda walio katika umoja unaotambuliwa na mamlaka za Serikali. Utaratibu huu unawawezesha madereva hao kuchangia huduma za afya kwa umoja wao na kunufaika na bima ya afya kupitia mtandao mpana wa vituo zaidi ya 7,700 vilivyosajliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuhudumia wanachama wake ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wanufaika ni akina nani?

Wanufaika ni waendesha bodaboda walio katika umoja, wenza wao na watoto wasiozidi wanne wa kuzaa au kuasili wenye umri chini ya miaka 18.

Madhumuni ya Mpango wa Boda Boda Afya

  • Kutoa fursa kwa waendesha bodaboda kujisajili na kunufaika na huduma za bima ya afya zinazotolewa na Mfuko;
  • Kulinda kipato cha waendesha bobaboda kwa kuwapa uhakika wa matibabu kupitia kadi ya bima ya afya.

Jinsi ya kujisajili na mambo muhimu ya kuzingatia

  • Mwanachama anatakiwa kujaza fomu ya kujiunga (inapatikana katika ofisi za Mfuko au tovuti ya Mfuko www.nhif.or.tz ) kupitia Uongozi wa Umoja/kikundi husika.
  • Kikundi au Umoja uwe umetambuliwa na mamlaka za Serikali.
  • Utaratibu huu utahusisha usajili wa kundi zima na siyo mwanachama mmoja mmoja na fomu za uanachama, viambatanisho na taarifa zote muhimu za wategemezi zitawasilishwa kwenye Mfuko kupitia Chama au Umoja wao.
  • Mchango wa kila mwanachama ni Shilingi 100,000 kwa mwaka. Aidha, mwanachama atamlipia mwenza Shilingi 100,000 na mtoto Shilingi 50,400 pindi atakapotaka kuwaunganisha.
  • Michango ya wanachama wote italipwa kwa mkupuo kupitia umoja husika.
  • Mwanachama anatakiwa kuwa na Kitambulisho cha Taifa au namba ya kitambulisho cha uraia wakati wa usajili.
  • Mwanachama atapata kitambulisho cha matibabu kwa kuzingatia vigezo na masharti ya mpango wa BODABODA AFYA.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na ofisi ya Mfuko iliyo karibu na wewe au wasiliana nasi kupitia simu ya huduma kwa wateja bila malipo 0800 110063