Chama cha Madaktari nchini kimesema kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ndio nguzo muhimu katika uimarishaji wa utoaji wa huduma za matibabu nchini.
Aidha Chama hicho kimesema hakiko tayari kuona NHIF ikifa kwa namna yoyote kutokana na umuhimu wake kwa Watanzania.
Hayo yamesemwa na Rais wa MAT, Dkt. Deuddedit Ndilanha katika kikao kazi kati ya MAT na NHIF kwa lengo la kujadili maboresho ya Kitita cha mafao kinachopendekezwa kuanza kutumika.
"Sisi MAT hatuwezi kutishia kuacha kutibu wanachama wa NHIF na hatuko tayari kuona Mfuko ukifa hata siku moja, NHIF imekuwa nguzo muhimu sana katika utoaji wa huduma za matibabu kwa Watanzania hivyo tutajadili na tutakubaliana namna bora ili wachama waendelee kupata huduma," alisema Dkt. Ndilanha.
Kwa upande wa Madaktari ambao ni viongozi wa Chama hicho, waliipongeza NHIF kwa ushirikishaji inayoufanya katika mabadiliko ama maboresho ya huduma za matibabu kwa wanachama wake.
Akifungua kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga alisema Mfuko unaamini katika dhana ya kushirikisha wadau wake wote katika maboresho inayoyafanya hivyo itatumia ushauri na maoni ya Chama hicho kuboresha zaidi kitita cha Mafao.
"Tunaamini sana katika kushirikishana kwa uwazi ili sote tuelewane na tutembee pamoja katika kuwahudumia wanachama wetu, maoni na ushauri wenu ni wa muhimu sana kwetu na tunaufanyia kazi," alisema Bw. Konga.
Mfuko unaendelea kukutana na wadau wake ili kufikia maamuzi sahihi ya uboreshaji wa huduma zake hususan kitita cha mafao.