Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Mazrui ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kwa kazi kubwa ya kuwahudumia wananchi na kuwafikia katika maeneo yao.
Mbali na hilo, amepongeza mashirikiano baina ya NHIF na Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) yanayowezesha wanachama wa ZHSF kuhudumiwa katika vituo vilivyosajiliwa na NHIF Tanzania Bara.
Hayo ameyasema leo ndani ya Banda la NHIF katika Maonesho ya Sabasaba ya Kimataifa ya 48 yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.
"NHIF mnafanya kazi nzuri sana katika utoaji wa huduma, mimi nimekuwa mwanachama wenu na nimefurahia huduma hivyo endeleeni kuwafikia wananchi kwa wingi zaidi ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu," alisema Mhe. Waziri.
NHIF katika maonesho haya inatoa huduma mbalimbali ikiwemo elimu, uhamasishaji, usajili wa wanachama wapya, kupokea maoni na kutatua changamoto za wanachama wanazokutana nazo wakati wa kupata huduma.