Wafikieni wananchi walipo wajiunge na NHIF- Muhimbi
Na Mwandishi NHIF- Mbeya
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeagizwa kuhakikisha unawafikia wananchi kwa kuwapa elimu na hatimaye kuwaandikisha kujiunga na Mfuko huo ili wapate uhakika wa huduma za matibabu.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF Bw. Juma Muhimbi wakati wa kuzindua Baraza la Tatu la Wafanyakazi wa NHIF lililofanyika Jijini Mbeya.
“Lengo la Serikali ni wananchi kuwa ndani ya bima ya afya hivyo hakikisheni kila mmoja kwa nafasi yake anatekeleza hilo. Wafikieni wananchi waliko muwapatie elimu ya huduma za Bima ya Afya na muwaandikishe na katika hili wekeni malengo ya kujipima,” alisema Bw. Muhimbi.
Mbali na hilo alitumia nafasi hiyo kukemea suala la udanganyifu linalofanywa katika huduma ambapo aliiagiza Menejimenti kulifanyia kazi zaidi kwa kubaini wanaojihusisha na vitendo hivyo na kuwachukulia hatua stahiki.
Naye Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Bw. Henry Mkunda ameipongeza NHIF kwa kazi inayofanya katika kuwahudumia wananchi kwa kuwa afya ndio mtaji mkubwa kwa kila mwananchi.
Akizungumzia Baraza la NHIF, alisema ni Baraza la mfano ambalo limesimama vizuri na Baraza ambalo linaendeshwa kwa kanuni hivyo kwa upande wa vyama wa wafanyakazi limekuwa ni Baraza la mfano na limekuwa kioo kwa mabaraza mengine.
Alisema kuwa kitendo cha ushirikishwaji wa Wafanyakazi wa NHIF umekuwa ni mkubwa katika maeneo yote hatua inayosaidia Menejimenti kupata hoja nyingi zinazolenga uboreshaji wa huduma za matibabu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga amesema kuwa katika kikao hicho mambo mbalimbali yamejadiliwa ikiwemo namna bora ya kuwafikia wananchi na kuboresha huduma za matibabu.
Mwisho.