TUNAPIMA NA KUTOA ELIMU YA AFYA BURE NANE NANE MBEYA- NHIF

TUNAPIMA NA KUTOA ELIMU YA AFYA BURE NANE NANE MBEYA- NHIF Aug 04, 2023

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), unawahimiza wananchi wa mkoa wa Mbeya na mikoa ya jirani kufika katika banda lake kwenye maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale ili kupata huduma za upimaji na elimu ya afya bure.

Rai hiyo imetolewa na Meneja Uhusiano wa NHIF Bi. Anjela Mziray ambaye ameeleza kuwa, suala la kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ni la msingi kwa kila mtu na Mfuko unachangia juhudi za Serikali kwa kutoa huduma za upimaji bure na kutoa elimu ya kuepukana na magonjwa hayo katika ushiriki wake kwenye maonesho ya Nanenane.

"Tupo hapa kwenye viwanja vya John Mwakangale ndani ya Mabanda ya Taasisi za Umma, tunawahimiza wananchi na washiriki wa maonesho haya kufika hapa na kupima na kujua hali za Afya zao na kupata elimu mtindo bora wa maisha ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza," alisema Anjela.

Vipimo vinavyofanyika bandani hapo ni pamoja na Shinikizo la damu, sukari na hali lishe na kisha kupatiwa elimu ya mtindo bora wa maisha ili kuepukana na magonjwa hayo.

Huduma zingine ni pamoja na usajili wa wanachama, elimu ya dhana ya bima ya afya, kupokea maoni na kushughulikia changamoto za wadau.

Akizungumzia ushiriki wa Mfuko katika maonesho ya Nane Nane, alisema Mfuko unashiriki maonesho ya Nanenane kikanda kwenye mikoa ya Mbeya, Tabora, Morogoro,Arusha, Lindi na Simiyu.

Kutokana na hayo, amewahimiza wananchi kutumia fursa hii kujiunga na kuwa na uhakika wa matibabu wakati wote.