Singida 16.01.2026
Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya (NHIF) umeanza rasmi kutekekeza ahadi ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ahadi ya kuanza mpanga wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kuanza zoezi la usajili wa wanachama wa makundi maalum.
Zoezi la limefanyika kwa kundi la Wazee wanaotunzwa katika nyumba ya Wazee iliyopo Sukamahela mkoani Singida. Usajili huo umeenda sambamba na kupewa kadi za bima ya afya ikiwa ni kiashirio cha utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Hatua hii ni muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa makundi maalum na kufikia azma ya serikali ya huduma bora kwa kila mtanzania.
Gharama za bima ya afya kwa kundi hili zinalipiwa na Serikali ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wote, hususan makundi yenye uhitaji maalum wanapata huduma bora za afya bila kikwazo cha fedha.
Katika zoezi hilo, jumla ya wazee 16 waliopo katika makazi hayo wamepatiwa kadi za bima ya afya.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Meneja wa Mfuko mkoa wa Singida Bw.Benjamin Mwalugaja alisema kuwa utoaji wa kadi hizo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya, hususan makundi yaliyo katika mazingira magumu kama vile wazee wasiojiweza.
Bw.Mwalugaja amesema “kundi hili limekuwa la kwanza mkoani Singida kupatiwa kadi hizo za bima ya afya na kupitia kadi hizo, wazee hao sasa wataweza kupata huduma mbalimbali za matibabu katika vituo vya afya vilivyosajiliwa na Mfuko, bila ya kikwazo cha kifedha ambapo mara nyingi imekuwa changamoto kubwa kwao”
Aliongeza kuwa Mfuko utaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha makundi mengine yanayostahili yanatambuliwa na kufikiwa kwa wakati.
Wazee wa kambi ya Sukamahela mkoa wa singida walipokea kadi hizo na kueleza furaha na kutoa shukrani kwa serikali na Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya kwa kuwaondolea mzigo wa matibabu na kwamba wamepata matumaini ya kuishi maisha yenye matumaini.
Hata hivyo viongozi wa wazee walipongeza juhudi za serikali kuendelea kujali na kuthamini makundi maalum na kwamba watatoa ushirikiano kwa serikali na Mfuko katika kuhakikisha kadi hizo zinatumiwa katika matumizi sahihi.
Kwa ujumla, zoezi hili ni mwanzo mzuri wa utekelezaji wa Sheria kwa kuanzia katika mkoa wa Singida, lakini litakuwa endelevu katika mikoa yote nchini na Mfuko unatarajia kuwafikia wazee na makundi mengine yote yenye mahitaji maalum.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge sasa