Ziara ya Bodi Ofisi ya NHIF Mkoa wa Mbeya, Watumishi waelekezwa kuongeza Usajili wa Wanachama

Imewekwa: 30 September, 2025
Ziara ya Bodi Ofisi ya NHIF Mkoa wa Mbeya, Watumishi waelekezwa kuongeza Usajili wa Wanachama

30/09/2025               Mbeya

Mwenyekiti wa msafara huo, Prof. George M. Ruhago aliwaasa watumishi wa NHIF kutumia fursa zilizopo kuongeza wanachama. Mbeya ni Mkoa Mkubwa kiuchumi na wenye fursa nyingi. Hivyo ni muhimu kutumia fursa hizo kusajili wanachama, alisisitiza Pro. Ruhago.

 Hivyo, aliwataka watumishi kuongeza juhudi ili kuleta matokeo chanya. Hapa kuna vyuo vingi, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wakulima pamoja na watumishi wa Sekta rasmi hivyo Bodi inatarajia matokeo makubwa.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi, CPA Dickson  mwingine wa A. Kaambwa, alisisitiza umuhimu wa malengo yanayowekwa kuwa na vipimo bayana vya ufanisi ili iwe rahisi kufanya tathmini na kubaini kiwango cha mafanikio pamoja na changamoto zilizojitokeza. Hata hivyo, aliwapongeza watumishi kwa jitihada wanazoendelea nazo katika kufanikisha malengo ya Mfuko.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Irene C. Isaka, aliipongeza ofisi hiyo kuendelea kutekeleza majukumu yao na akawataka waendelee kuongeza ufanisi. Pia aliwasisitiza kuimarisha uhamasishaji kwa wajasiriamali, kutumia fursa za majukwaa kama AMCOSS, kushirikiana na benki, na mawakala waliosajiliwa ili kuhakikisha angalau asilimia 10 ya wananchi wa Mkoa wa Mbeya wanajiunga na bima ya afya.

Dkt. Isaka aliwahimiza watumishi kujituma zaidi, akibainisha kuwa utekelezaji wa bima ya afya kwa wote unahitaji matokeo ya haraka, hasa katika mikoa mikubwa kama Mbeya ambayo ni kitovu cha ukanda wa nyanda za juu kusini.

Bima ya Afya kwa Wote. Jiunge Sasa