Wekeni mkazo kwenye utoaji wa elimu- Bodi NHIF

Imewekwa: 12 August, 2025
Wekeni mkazo kwenye utoaji wa elimu- Bodi NHIF

Na Mwandishi Wetu, Kagera

Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), imeziagiza Ofisi zote za Mfuko kuweka mkazo katika utoaji wa elimu ya bima ya afya kwa wananchi ili wafahamu manufaa yake hatua itakayowezesha kujiunga na kuongeza idadi ya wanachama.

Agizo hilo limetolewa leo na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi Dkt. Zubeda Chande wakati wa hitimisho la ziara ya Bodi hiyo katika mikoa ya Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mara, Mwanza, Geita na Kagera. Dkt. Chande ameongozana na Wajumbe wa Bodi Bw. Amour Amour na Bw. Shaban Kabunga.

Katika ziara hiyo, Bodi ya NHIF imefanikiwa kukutana na Wakuu wa Mikoa na kuweka mikakati ya kuwafikia wananchi katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, kupata mrejesho wa huduma toka kwa wanachama na kuimarisha mahusiano ya Mfuko na Serikali za Mikoa.

Alisema kuwa katika kipindi hiki ambacho Serikali inataka wananchi wake wawe na bima ya afya, ni vyema kila ofisi ikaongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo njia zinazohusisha utamaduni wa mkoa husika ili kurahisisha ufikishaji wa elimu hiyo.

“Serikali inatuangalia na inahitaji tuwafikie wananchi na kuwasajili ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha, kwa upande wake Serikali imefanya kazi kubwa ya kuwekeza katika vituo kwa kuweka vifaa tiba vya kisasa, dawa na miundombinu hivyo kinachotakiwa ni sisi kuwafikia wananchi na kuwasajili ili wanufaike na huduma hizo,” alisema Dkt. Chande.

Bodi ya Wakurugenzi yakutana na Watumishi wa Mfuko Ofisi ya Mkoa wa Kagera

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Isaka aliwataka Watumishi kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha anajituma kutokana na malengo yaliyowekwa ili kufanikisha matamanio ya Serikali.

“Kwa Watumishi wote hususan mlioko huku mikoani, nawaomba sote tuwe na mtazamo chanya wa kuwepo huku kwa kuwa tumeaminiwa kuwahudumia wananchi hivyo kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anatekeleza majukumu yake ipasavyo kwa weledi na kwa kuzingatia taratibu na miongozo iliyopo,” alisema Dkt. Isaka.

Kwa upande wa Ofisi za Mikoa hiyo, kwa pamoja wameiahidi Bodi kufanya kazi kwa kujituma ili lengo la kuwasajili wananchi katika meneo yote liweze kufikiwa.

Mfuko kwa sasa umesogeza zaidi huduma kwa wananchi kwa kuwa na Ofisi kila Mkoa lakini pia imefanikiwa kufungua Ofisi katika maeneo ya kimkakati ambayo ni pamoja na Ifakara mkoani Morogoro, Karagwe mkoani Kagera, Kahama mkoani Shinyanga, Bukombe mkoani Geita, Tegeta mkoani Dar es Saalam na Nzega mkoani Tabora. Lengo kubwa la Ofisi hizi ni kusogeza huduma zaidi kwa wananchi na kufanikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.

Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa