Waziri wa Nchi - Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. Deus Sangu, ametoa pongezi kwa?Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa juhudi kubwa zinazofanywa katika kuhakikisha wananchi wengi wanawezeshwa kupata bima ya afya na huduma bora za matibabu.
Akizungumza wakati alipotembelea banda la NHIF kwenye mkutano wa wadau wa Sekta ya Kinga ya Jamii, Mhe. Sangu amesema hatua zinazochukuliwa na NHIF zinaendana kikamilifu na *maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuhakikisha wanapata **bima ya afya kwa wote*, hivyo kuwaondolea wananchi mzigo wa gharama za matibabu wanapokumbwa na changamoto za kiafya.
Aidha, Mhe. Sangu amesisitiza umuhimu wa Mfuko kuendelea kuongeza juhudi za uelimishaji, uhamasishaji na uandikishaji ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi, hususan walioko maeneo ya vijijini na makundi yaliyo katika sekta idiyo rasmi. Ameeleza kuwa upanuzi wa mpango wa bima ya afya kwa wote utawapa wananchi *uhakika wa matibabu wakati wote*, hivyo kuongeza tija katika uzalishaji na kuchangia ustawi wa jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake Meneja wa NHIF Mkoa wa Arusha Bw. Hipoliti Lelo, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko Dkt. Irene Isaka, akitoa maelezo kwa Mhe Waziri alisema NHIF inaendelea kutekeleza majukumu ya Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote pamoja na sasa Mfuko upo katika utekekezaji wa jukumu la kusajiri wanachama toka kaya zisizo na uwezo nchi nzima, ikiwa na awamu ya kwanza ya zoezi.
Vilevile, Lelo alimhakikishia Mhe. Waziri kuwa NHIF inaendelea na programu ya kutoa elimu kwa umma ili makundi mbalimbali ya Watanzani waweze kujiunga na Mfuko ili wanufaike na bima ya afya.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa