WANANCHI WANUFAIKA NA HUDUMA ZA NHIF KATIKA MAONESHO YA OSHA NJOMBE

Imewekwa: 30 April, 2026
WANANCHI WANUFAIKA NA HUDUMA ZA NHIF KATIKA MAONESHO YA OSHA NJOMBE

Wananchi wameendelea kupata huduma mbalimbali za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika banda la NHIF lililopo kwenye maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema, mkoani Njombe.

Kupitia banda hilo, wananchi wamepata huduma muhimu za uanachama ikiwemo kujisajili kujiunga na NHIF, kuhuisha taarifa zao, kuongeza wategemezi pamoja na kupatiwa elimu kuhusu vifurushi mbalimbali vya bima ya afya vinavyotolewa na Mfuko. Huduma hizo zimetolewa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa bima ya afya na kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuwa na kinga ya matibabu.

Maafisa wa NHIF kutoka Ofisi ya Mkoa wa Njombe wamekuwepo kutoa huduma hizo kwa ufanisi, wakisaidiana na wanamichezo wa NHIF walioungana nao katika kuwahudumia wananchi pamoja na kutoa elimu ya afya. Ushirikiano huo umeongeza hamasa na kuvutia wananchi wengi zaidi kufika katika banda hilo.

Wananchi waliotembelea banda hilo wamepongeza juhudi za NHIF kwa kusogeza huduma karibu nao, huku wakieleza kuwa elimu waliyoipata imewasaidia kuelewa zaidi faida za bima ya afya katika kukabiliana na gharama za matibabu.

Ushiriki wa NHIF katika maonesho ya OSHA unaendelea kuwa muhimu kwa lengo la kufikisha huduma na elimu kwa jamii, sambamba na kuhamasisha umuhimu wa afya na usalama katika maisha ya kila siku.

Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa!