16 Julai, 2025 Dodoma
Wajumbe wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Bahari na Meli (DOWUTA) kutoka Bandari ya Dar es Salaam, kitengo cha Makasha kinachofahamika kama *Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL)*, wametembelea ofisi za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Makao Makuu kwa lengo la kupata elimu ya bima ya afya na kuwezesha usajili wa zaidi ya wafanyakazi 500 wa kampuni hiyo kwenye Mfuko wa NHIF.
Ujumbe huo ulipokelewa na *Mkurugenzi wa Huduma za Uanachama wa NHIF, Dkt. Alphonse Chandika*, ambaye alieleza kuwa hatua hiyo ni ya kupongezwa, kwani inachangia kwa kiasi kikubwa jitihada za Mfuko katika kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanajiunga na kupata huduma za bima ya afya.
"Lengo letu kama NHIF ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kupitia bima, na uamuzi wa TEAGTL kujiunga nasi ni hatua kubwa kuelekea azma ya bima ya afya kwa wote," alisema Dkt. Chandika.
Kwa upande wa ujumbe wa TEAGTL, *Katibu wa DOWUTA, Paschal Lugaga*, aliyemwakilisha Mwenyekiti wa chama hicho, alishukuru kwa mapokezi mazuri na kueleza kuwa lengo la chama ni kuhakikisha kuwa wafanyakazi pamoja na wategemezi wao wanapata huduma bora za afya kupitia NHIF.
"Tumeamua kujiunga na NHIF kwa sababu ni taasisi kubwa, yenye uzoefu na inayotoa huduma bora za bima ya afya nchini. Tunaamini kupitia NHIF, tutapunguza gharama za matibabu kwa watumishi wetu na kuongeza ufanisi wa kazi," alisema Lugaga.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa pande zote mbili kufikia makubaliano juu ya kuanza mara moja mchakato wa usajili wa kampuni hiyo kwenye mfumo wa NHIF, hatua inayotarajiwa kuwanufaisha wafanyakazi wengi pamoja na familia zao.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa