Na Mwandishi Wetu, Arusha
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dkt. Irene Isaka amesema Mfuko utashirikiana katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote na vyama mbalimbali vya kitaalam ili kuwezesha utoaji wa huduma ulio bora zaidi.
Dkt. Isaka ameyasema hayo jana wakati akiwasilisha mada kwenye Kongamano la Kisayansi la Chama cha Madaktari Tanzania lililolenga kuadhimisha miaka 60.
Alisema kuwa kazi kubwa iliyofanywa na Mfuko katika maandalizi ya utekelezaji wa Bima ya Afya kWa wote ni ushirikishwaji wa wadau mbalimbali wakiwemo madaktari kupitia vyama vyao.
“Tulianza na utoaji wa elimu kwa wadau muhimu ambayo iliambatana na kupata maoni ya namna gani huduma zitolewe na huduma zipi kwa wanachama, pamoja na kukamilisha hili lakini tutaendelea kushirikiana nanyi na wataalam wengine ili utoaji wa huduma kwa wanachama wetu uwe bora zaidi.
Picha ya pamoja ya viongozi na washiriki wa Kongamano la kisayansi la maadhimisho ya miaka 60 ya Chama cha Madakitari Tanzania linalofanyika jijini Arusha
Katika hatua nyingine, Dkt. Isaka alitoa wito kwa wadau hao kulinda huduma na kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu wakati wakitoa huduma kwa wanachama wa NHIF.
Kwa sasa Mfuko unaendelea na usajili wa Wanachama wake kupitia kifurushi cha Tarangire ambacho kimeboreshwa kwa kuongezwa huduma mbalimbali za msingi na za kitaalam zaidi.
BIMA YA AFYA KWA WOTE, JIUNGE SASA