TUHAMASISHE WANAFUNZI KUJIUNGA NA BIMA YA AFYA MASHULENI - MSIGWA

Imewekwa: 21 June, 2025
TUHAMASISHE WANAFUNZI KUJIUNGA NA BIMA YA AFYA MASHULENI - MSIGWA

Katika Maonesho ya UTAMADUNI, BULABO yanayofanyika mkoani Mwanza, Katibu Mkuu na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa, ametembelea banda la NHIF na kutoa wito kwa shule za serikali kuhamasisha wanafunzi wao kujiunga na bima ya afya kupitia mashuleni.

Ndg. Msigwa amesema kuwa hatua hiyo italeta tija kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla kwani itawajengea utamaduni wa kulinda afya zao tangu wakiwa wadogo. Ameeleza kuwa bima ya afya ni msingi imara wa maendeleo na ustawi wa wananchi hasa watoto ambao ndio taifa la kesho.

“Tukiwajengea watoto wetu utamaduni wa kuwa na bima ya afya tangu wakiwa shuleni, tunawaandaa kuwa raia wanaojali afya na wanaoweza kukabiliana na changamoto za kiafya bila kutetereka,” amesema.

Amepongeza NHIF kwa kuendelea kutoa elimu na huduma bora kwa jamii na kuhimiza wazazi, walimu na viongozi wa elimu kushirikiana kuhakikisha kila mwanafunzi anapata bima ya afya.

Katibu Mkuu na Msemaji wa Mkuu wa Serikali, Ndg,Gerson Msigwa akipata maelezo ya huduma za NHIF katika maonesho ya Utamaduni BULABO yanayofanyika jijini Mwanza.

\#NHIF #BimaYaAfyaKwaWote #UTAMADUNIBULABO2025 #GersonMsigwa #BimaMashuleni #Mwanza