Na Grace Michael, Shinyanga
Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), imewataka Watumishi kuachana na utendaji kazi wa mazoea na badala yake wajielekeze kwenye utendaji kazi wenye matokeo na unaozingatia utoaji bora wa huduma kwa wanachama wake.
Agizo hilo limetolewa jana katika mikoa ya Shinyanga na Tabora na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bi. Zuena Chande wakati akizungumza na Watumishi wa NHIF mikoani humo.
Alisema kuwa katika kipindi hiki ambacho Serikali ina matarajio makubwa na NHIF katika kuwafikia wananchi wote kupitia Bima ya Afya kwa Wote, ni lazima kila Mtumishi abadili mtazamo wake katika kazi ili kuweza kufanikisha malengo yaliyowekwa.
Bi. Chande aliwataka watumishi kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii, maarifa, uadilifu na ubunifu unaohusisha uelimishaji unaotumia njia sahihi katika eneo husika kwa kuzingatia utamaduni na shughuli za kiuchumi za eneo hilo ili kuwezesha kufikisha elimu tarajiwa kwa haraka na kupata mapokeo Chanya.
Baadhi ya Watumishi wa Mfuko wakiwa katika kikao na wajumbe wa Bodi walipofanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kuzungumza na watumishi wa Mfuko.
“Niwaombe sana tukikutana na changamoto yoyote iliyoko nje ya uwezo wenu iwasilisheni kwa Menejimenti ili iwasadie kuitatua na inaposhindwa sisi Bodi tupo kuhakikisha tunafanyia kazi ili msikwame katika kuwafikia na kuwahudumia wananchi,” alisema Bi. Chande.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi Bw. Amour Amour aliwataka Watumishi kuweka mikakati itakayowezesha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ili kutimiza azma ya Serikali ya wananchi wote kuwa ndani ya Mfumo wa Bima ya Afya.
Wakielezea mikakati waliyoiweka Mameneja wa Mkoa wa Tabora na Shinyanga, wameihakikishia Bodi kuwa wamejipanga kuwasikia wananchi wa ngazi za chini zaidi kwa kushirikiana na Watendaji wa Serikali za vijiji, Wahudumu wa Afya na Mawakala waliosajiliwa na Mfuko kusajili wananchi.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu Dkt. Irene Isaka, alisema kuwa kazi kubwa iliyoko mbele yake ni kutekeleza maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuwasajili wananchi ili waweze kupata huduma za matibabu kupitia mfumo wa bima ya afya.
Dkt. Isaka alisisiza utoaji wa huduma bora kwa wanachama unaozingatia maadili na Weledi kwa kuwa huduma zinazotolewa na Mfuko zinahusisha maisha au uhai wa wanachama.
Ziara hii ni mwendelezo wa Ziara zinazofanywa na Bodi ya Wakurugenzi kwa lengo la kupata mrejesho wa huduma na kujionea mazingira ya kazi waliyonayo Watumishi pamoja na kutatua kero wanazokutana nazo katika kuwahudumia wanachama.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa