Na Mwandishi Wetu, Singida
Serikali kupitia Wizara ya Elimu imeombwa kutoa mwongozo maalum utakaowawezesha wanafunzi wa shule za awali, msingi na sekondari kujiunga na Bima ya Afya, hatua inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa uhakika kwa kundi hilo.
Ombi hilo limetolewa na watumishi wa Mfuko wa Bima ya Afya Mkoa wa Singida wakati wa ziara ya Bodi ya Wakurugenzi iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za mfuko huo mkoani humo.
Akiwasilisha hoja hiyo kwa niaba ya watumishi, Meneja wa Mkoa, Bw. Benjamini Mwalugaja, alisema kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo katika usajili wa wanafunzi ni mfumo wa hiari uliopo sasa, tofauti na wanafunzi wa vyuo vikuu ambao tayari wana mwongozo unaowalazimu kujiunga na bima ya afya.
Alifafanua kuwa hali hiyo imekuwa kikwazo kikubwa katika kufikia idadi kubwa ya wanafunzi, hivyo kusisitiza umuhimu wa Serikali kutoa mwongozo utakaoweka usajili wa lazima kwa wanafunzi wa ngazi hizo za elimu.
“Tunaiomba Bodi iangalie namna ya kuishauri Serikali kupitia Wizara ya Elimu ili kutoa mwongozo kama ilivyo kwa wanafunzi wa vyuo. Hii itasaidia kuongeza wigo wa wanafunzi,” alisema Bw. Mwalugaja.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF, Bw.Eliud Sanga akisaini kitabu cha Wageni akiwa mkoani Singida katika ziara ya kikazi.
Akizungumza na watumishi hao, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Bw. Eliud Sanga, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuahidi kuwa Bodi itaifanyia kazi kwa kushirikiana na Serikali ili kupata suluhisho la kudumu.
Alisisitiza kuwa bado kuna kazi kubwa ya kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanajiunga na bima ya afya, ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za matibabu bila kikwazo cha kifedha.
Katika kuimarisha uhamasishaji, Bw. Sanga aliwataka watumishi kutumia mikusanyiko mikubwa ya wananchi, hususan nyumba za ibada, kama jukwaa la kutoa elimu kuhusu umuhimu wa bima ya afya.
“Nyumba za ibada ni sehemu muhimu ambapo wananchi hukusanyika kwa wingi na kuamini viongozi wao. Tutumie fursa hii kuwaelimisha juu ya faida za kujiunga na bima ya afya na namna inavyosaidia kuepuka changamoto za matibabu,” alieleza.
Katika hatua nyingine, Bw. Sanga aliwahimiza watumishi kutumia muda wao wa kazi kwa ufanisi na kujihusisha na shughuli za kiuchumi baada ya muda wa kazi ili kujiongezea kipato na kuimarisha maisha yao.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi, Profesa George Luhago, alisisitiza umuhimu wa ufuatiliaji wa karibu wa matumizi ya huduma za afya kwa wanachama, pamoja na kuhakikisha ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo vya afya.
Aliwataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii huku akiwapongeza kwa mchango wao mkubwa katika kuboresha huduma kwa wananchi.

Watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoa wa Singida wakifuatilia kikao wakati wa ziara ya bodi ya wakurugenzi mkoani humo tarehe 13/04/2026.
“Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge sasa.”