Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa maboresho makubwa yaliyofanyika hususan ya kuwafikia wananchi na kuwapa huduma bora.
Hayo aliyasema jana alipokutana na Menejimenti ya NHIF iliyoongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Irene Isaka kwa lengo la kupata mrejesho wa huduma na namna Mfuko ulivyojipanga kuwafikia wananchi hususan katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote pamoja na huduma zinazotolewa na Mfuko kwa Skimu ya Bima ya afya kwa Wabunge
Mhe. Dkt. Tulia alisisitiza umuhimu wa Mfuko kuendelea kutatua changamoto zinazojitokeza na kuleta vikwazo kwa wananchi kujiunga na bima ya afya.
“Kwanza kabisa nikupongeze sana Mkurugenzi Mkuu kwa mabadiliko makubwa ya kihuduma uliyoyafanya kwa muda mfupi na kuwa na mafanikio yanayoonekana, niwasisitize tu muendelee kuangalia na kushughulikia changamoto zilizopo ili wananchi wasikwame kujiunga na huduma,” alisema Mhe. Spika.
Akizungumzia maboresho yanayoendelea kufanyika ndani ya Mfuko, Dkt. Isaka alisema kuwa kipaumebele cha Mfuko kutumia Mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha usajili wa wanachama, ukusanyaji michango pamoja na uchakataji wa madai ili kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara.
Aidha, alieleza hatua iliyofikiwa na Mfuko katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ambapo alisema tayari usajili wa makundi ikiwemo wanafunzi umeshaanza kufanyika Pamoja na watu binafsi hivyo utoaji wa elimu unaendelea kuhakikisha kila mwananchi anajiunga na bima ya afya.
Alimhakikishia Mhe. Spika kuwa, Mfuko umeimarisha upatikanaji wa huduma bora za matibabu kwa wananchi nchini pamoja na kuwa na mfumo imara wa kujibu au kushughulikia changamoto zao kwa haraka.
Akizungumzia huduma zinazotolewa na NHIF kwa Bunge, Dkt. Isaka alisema kuwa, Mfuko umefanikiwa kuhudumia chombo hicho kwa muda wa miaka 10 hivyo akaahidi uboreshaji zaidi wa huduma kwa kundi la Waheshimiwa wabunge ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu kwao pamoja na wategemezi wao wakati wowote.