Dar es Salaam
Na Mwandishi Wetu
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeingia makubaliano rasmi ya kutoa huduma za bima ya afya kwa wafanyakazi wote wa PUMA ENERGY TANZANIA, kampuni kubwa katika sekta ya nishati hapa nchini.
Bwana Cannon Luvinga, Meneja wa NHIF Mkoa wa Temeke, alimhakikishia Mkurugenzi Mkuu wa PUMA ENERGY TANZANIA, Bi. Fatma Abdallah, kuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo watapata huduma bora za matibabu katika vituo vyote vya afya vilivyosajiliwa na NHIF.
"NHIF ndio mtoa bima pekee mwenye mtandao mkubwa zaidi wa vituo vya afya nchini, hakuna mtoa bima mwingine yeyote aliyetufikia. Kwa sasa, tuna zaidi ya vituo 10,000 vilivyosajiliwa vinavyotoa huduma kwa wanachama wetu na wategemezi wao," alisema Bw. Luvinga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PUMA ENERGY TANZANIA alishukuru kwa uhusiano huu mpya, akasisitiza imani yake kwa NHIF na kutarajia huduma thabiti za afya kwa wafanyakazi na wategemezi wao. Alibainisha kuwa makubaliano haya yataimarisha utendaji kazi kwa kuhakikisha upatikanaji wa matibabu bora.