Dar es Salaam
Na Mwandishi Wetu
Kwa lengo la kuhakikisha elimu ya Bima ya Afya kwa Wote inafikia Watanzania wote, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kupitia Ofisi yake ya Mkoa wa Temeke ilitoa mada maalum kuhusu Bima ya Afya Kwa Wote kwa waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke leo Jumanne tarehe 27 Mei 2025.
Wakati akitoa mada hiyo, Meneja wa Ofisi ya NHIF Temeke Bwana Cannon Luvinga aliwahimiza madiwani kuhakikisha wanafikisha elimu hii katika maeneo yao. Alisisitiza kwamba ikiwa kila Diwani atatumia vyema elimu hii, serikali itafanikiwa katika azma yake ya kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na bima ya afya, na hivyo kuondoa vikwazo katika kupata huduma za matibabu.
"Serikali imejitolea kikamilifu kuhakikisha kila Mtanzania anajiunga na bima ya afya, kwa mtu mmoja mmoja au kwa kaya nzima, kwa gharama nafuu. Kwa kaya zisizo na uwezo wa kumudu gharama hizo, serikali itazitambua na kusaidia kulipa ada zao ili kuhakikisha hakuna aliyeachwa nyuma kwa sababu za kifedha," alisema Bwana Luvinga.
Kikao hicho kiliongozwa na Meya wa Halmashauri ya Temeke Mheshimiwa Abdallah S. Mtinika, ambaye alishukuru NHIF kwa kuona umuhimu wa kuwahusisha madiwani katika kueneza elimu hii. Aliwaagiza wajitahidi kuhamasisha mpango huu katika maeneo yao ili idadi ya wanachama iongezeke, kulingana na malengo ya serikali ya bima ya afya kwa wote.
"Elimu hii lazima ifikie kila mwananchi wa Wilaya ya Temeke ili idadi ya wanaojiunga iendelee kuongezeka kwa mujibu ya maono ya serikali," alisema Meya Mtinika.
Mwisho.