Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego ameahidi kufanya kampeni maalum kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya ili kufikia matarajio ya Serikali ya kila mwananchi kutibiwa kwa utaratibu wa Bima ya Afya.
Hayo ameyasema leo katika banda la NHIF kwenye Maonesho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani yanayofanyika Kitaifa Mkoa wa Singida.
"Kwanza niwapongeze NHIF kwa maboresho makubwa ya kihuduma mliyoyafanya baada ya maonesho haya tuanze kampeni maalum ya kuwahamasisha wananchi katika maeneo yote ili wajiunge kwa wingi na kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wote,"alisema Mhe. Dendego.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa (CCM), Mhe. Martha Mlata amepongeza hatua iliyofikiwa na NHIF kwa sasa katika utoaji wa huduma kwa wananchi ikilinganishwa na hapo awali.
"NHIF mnastahili pongezi kubwa kwa namna mnavyotoa huduma kwa sasa, mmefanya maboresho makubwa yaliyorahisisha upatikanaji wa huduma zenu, binafsi ni mdau wenu mkubwa na ninafurahia huduma mnazotoa," alisema Mhe. Mlata.
NHIF inashiriki maonesho hayo kwa kutoa huduma ya elimu ya bima ya afya kwa wananchi lakini pia kusajili wanachama na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo.
BIMA YA AFYA KWA WOTE, JIUNGE SASA