Na Mwandishi Wetu, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anamringi Macha amesema yuko tayari kuongozana na Maofisa wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kwenda kutoa elimu kwa wananchi ili wajiunge na bima ya afya.
Amesema kuwa ili kuepukana na gharama kubwa za matibabu zinazosababisha wananchi kuingia kwenye umasikini na wakati mwingine kupoteza maisha ni kujiunga na bima ya afya ambayo inawezesha kupata matibabu bila kikwazo cha fedha.
Ahadi hiyo ameitoa mbele ya Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF iliyotembelea ofisini kwake kwa ajili ya kuweka mikakati ya kuwafikia wananchi wakati wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote pamoja na kuimarisha mahusiano ya Serikali ya Mkoa na NHIF.
Alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo kwa upande wa wananchi wa Simiyu ni uelewa wa dhana ya bima ya afya hivyo akaahidi kuongozana na Maofisa wa NHIF kwenye mikutano mbalimbali ya wananchi ili watoe elimu ba kuhamasisha.
“Wananchi wa hapa uwezo wa kujiunga na bima ya afya wanao isipokuwa uelewa wa bima ya afya uko chini sana hivyo ni lazima tuwe na mkakati wa kukuza uelewa ili wananchi wajiunge ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha,” alisema Mhe. Macha.
Alisema kuwa njia nyingine itakayowezesha ushawishi wa wananchi kujiunga ni pamoja na kuzingatia tamaduni za wananchi wa Simiyu ili kuwezesha mapokeo chanya.
Mhe. Macha alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa NHIF kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha malengo ya Serikali ya kila mwananchi kuwa na bima ya afya yanafikiwa.
Menejimenti ya Mfuko wakiw akatika picha ya pamoja na Mhe.Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha walipotembelea ofisini kwake wakiwa katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu mapema wiki hii
Kwa upande wa Bodi ya NHIF, iliyoongozwa na Kaimu Mwenyekiti Bi. Zubeda Chande aliushukuru uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Simiyu kwa kukubali kushiriki katika uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa wananchi ili waweza kujiunga na bima ya afya.
Akitoa maelezo ya awali, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Irene Isaka alisema kuwa Mfuko umeweka mikakati mingi ya kuwafikia wananchi ikiwemo kutumia mawakala kusajili wananchi.
“Serikali yetu ina matarajio makubwa sana katika utekelezaji wa Bima ya Afya kWa Wote hivyo tutahakikisha tunatumia mbinu zote ikiwemo kubotesha huduma ili wananchi wajiunge na wafurahie huduma,” alisema Dkt. Isaka.
Ziara ya Bodi katika mikoa ya Tabora, Shinyanga na Simiyu imelenga kuimarisha mahusiano na kuweka mikakati thabiti ya kuwafikia wananchi katika maeneo yao na kuwahamasisha kujiunga na NHIF.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge sasa