Na Mwandishi Wetu Arusha 23 Julai, 2025
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Umepongezwa kwa kuimarisha mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha huduma kwa Wanachama na Wadau pamoja kusaidia kudhibiti udanganyifu unaoweza kufanywa na watoa huduma dhidi ya Mfuko hatua inayolenga kulinda uhai na uendelevu wa Mfuko.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhandisi Zena Ahmed Said alipotembelea banda la NHIF katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa mwaka wa Jumuiya za Wataalam wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala katika Utumishi wa Umma Tanzania (TAPA-HR), mkutano unaofanyika Jijini Arusha Katika Ukumbi wa kituo cha Mikutano cha kimataifa (AICC).
Mkurugenzi wa Huduma za uanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Dkt. Alphonce Chandika akiwa katika Ufunguzi wa Mkutano nkuu wa kwanza wa mwaka wa wataalam wa Utawala na Rasilimali Watu unaofanyika jijini Arusha katika Ukumbi wa kituo cha Mikutano AICC.
Kwa upande wa Meneja wa NHIF mkoa wa Arusha Bw. Hipoliti Lello alisema Mkuko unashiriki katika mkutano huo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu huduma na maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Mfuko hasa katika eneo la usajili wa wanachama kupitia Mfumo wa Self- Services.
Aidha kupitia maboresho haya yanasadia kuweza kutambua uhalali wa mwanachama kutokana na mifumo ya Mfuko kuunganishwa na mifumo ya mamlaka mbalimbali zikiwemo za NIDA na RITA. Uwezo wa Mifumo kusomana inasaidia kuzua udanganyifu. Kutokana na maboresho hayo, kwa kuwa sasa mwanachama anaweza kutumia Namba ya kitambulisho cha taifa kujisajili na kupata huduma.
Maofisa wa Mfuko wakiendelea na utoaji wa elimu ya usajili wa wanachama kupitia huduma ya self services.
Mkutano huu umewakutanisha wataalam zaidi ya 900 kutoka Wakala wa Serikali, Taasisi za Umma, Wizara, Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao wanasimamia Rasilimali Watu na Utawala. Mkutano huo unafanyika kuanzia tarehe 22 hadi 25 Julai, 2025.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa