Na Mwandishi Wetu
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umesema unashirikiana na hospitali ya kanda ya Benjamin Mkapa iliyopo mkoani Dodoma ili kufanikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia matibabu ya upandikizaji wa Uloto kwa Watoto wenye ugonjwa wa Selimundu (sickle Cell) pamoja na upandikizaji wa figo kwa wagonjwa wenye uhitaji.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Tiba na Huduma za Kitaalam toka NHIF, Dkt. David Mwenesano kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko Dkt. Irene Isaka wakati wa kutambulisha kwa Waandishi wa Habari zoezi la harambee ya kuchangia fedha za matibabu ya Selimundu na Figo.
Dkt. Mwenesano aliupongeza uongozi wa BMH kupitia Mtendaji wake Mkuu Prof. Abel Makubi kwa kuja na wazo la kuokoa maisha ya Watoto wenye ugonjwa wa Selimundu na wananchi wenye uhitaji wa kupandikizwa figo, magonjwa ambayo ni gharama kubwa kutibu.
“Kwa kutambua gharama za matibabu haya ni kubwa na siyo rahisi kwa Mtanzania wa kawaida kumudu, hivyo njia hii ya uchangiaji kupitia harambee inatoa fursa kwetu sote kushiriki.
Mwanzoni mwa suala hili wakati Mkurugenzi Mtendaji wa BMH anatafuta njia za kusaidia kuwezesha matibabu hayo alitushirikisha, hivyo sisi kama NHIF tukuwa wadau wakubwa wa sekta ya afya tukaona ni vyema kushirkiana na BMH ili kufanikisha upatikanaji wa fedha hizi,” alisema Dkt. Mwenesano.
Aliendelea kusema kuwa Mfuko umekuwa ukigharamia baadhi ya huduma katika magonjwa hayo, hivyo kutokana na ukubwa wa gharama zake Serikali imekuwa ikibeba gharama kubwa, hivyo harambee hii itasaidia kupanua huduma hizi na kuwafikia wagonjwa wengi zaidi.
Kutokana na hilo, alisema kuwa Mfuko umeendelea kufanya maboresho mbalimbali katika huduma zake ikiwemo ya kubuni vifurushi ambavyo vinatoa fursa kwa kila Mtanzania kuwa na Bima ya Afya hususan katika kipindi hiki ambacho tunatekeleza Bima ya Afya kwa Wote. Maboresho mengine ambayo yanafanyika ni pamoja na kuendelea kuongeza huduma za Matibabu kwenye Kitita kulingana na uwezo wa Mfuko, zaidi ya hayo ni uboreshaji wa mifumo mbalimbalu inayorahisisha kazi za Mfuko.

Mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya Kanda ya Benjamini Mkpaka akizungumza na vyombo vya habari katika mkutano wa vyombo vya habari wa maandalizi ya harambee ya kuchangia gharama za kupandikiza uloto
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa BMH, Prof. Makubi alisema kuwa huduma za upandikizaji Uloto kwa Watoto wenye ugonjwa wa Sickle Cell katika hospitali hiyo zilianza mwaka 2023 kwa kliniki ya kutoa matibabu kwa Wagonjwa wenye magonjwa ya damu na Wanaohitaji huduma za upandikizaji Uloto.
Alisema idadi ya watoto 28 wamepandikizwa uloto kwa jumla ya Sh. 1.9 Bilioni huduma ambayo imesaidia kuokoa shilingi 1.3 Bilioni kama matibabu haya yangefanyika nje ya nchi.
Prof. Makubi alisema kuwa malengo ya ukusanyaji wa fedha kupitia harambee ni kiasi cha shilingi Bilioni 7 ambazo zitaweza kusaidia wagonjwa 100, wakiwemo 50 wa kupandikiza Uloto na 50 wa kupandikiza figo.
Alisema kuwa harambee hiyo imepangwa kufanyika Mwezi Mei 08, 2026 Dodoma ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ili kufanikiwa hilo, ametoka rai kwa Mashirika, Taasisi, Makampuni, Wananchi wote na Wadau mbalimbali kushiriki katika kusaidia matibabu ya upandikizaji Uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa Selimundu na upandikizaji Figo kwa wananchi wenye uhitaji kwa kuchangia fedha kupitia njia zifuatazo: Control Namba 995220798235 Jina: BMH Organ Transplant na Account Namba 102501000407 (BOT) Jina: BMH Organ Transplant.

Mkutano na waandishi wa habari wa maandalizi ya harambee ya kuchangia gharama za upasuaji wa uloto kwa watoto 50 wenye changamoto ya Selmundu.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa