Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umetoa mafunzo elekezi ya siku nne kuanzia tarehe 23 hadi 26 jijini Dodoma kwa watumishi wapya yenye lengo la kuwajengea uelewa kuhusu maadili ya Utumishi wa Umma pamoja na umuhimu wa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zinazoongoza utumishi wa umma nchini.
Mafunzo hayo yanalenga kuwasaidia watumishi hao wapya kuanza majukumu yao kwa ufanisi, uwajibikaji na kuzingatia misingi ya utumishi wa umma ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bw. Lembris Laanyuni, aliwapongeza watumishi hao kwa kuwa sehemu ya timu ya NHIF, huku akiwataka kutumia fursa hiyo vizuri kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na nidhamu.
Bw. Laanyuni alisisitiza kuwa utumishi wa umma unahitaji uzingatiaji mkubwa wa maadili, uwajibikaji na kujituma ili kuhakikisha taasisi inatimiza malengo yake ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, aliwataka watumishi hao kuwa mabalozi wazuri wa Mfuko kwa kuishi misingi na tamaduni za Mfuko.
Aliendelea kusema kuwa NHIF imekabidhiwa dhamana kubwa ya utekelezaji wa Sheria ya bima ya afya kwa wote hivyo wao pia ni sehemu ya timu ya kufanikisha majukumu hayo ya kuhakikisha wananchi wote wanapata bima ya afya.
Kwa upande wake mwezeshaji kutoka chuo cha utumishi wa Umma Dkt.Emmanuel Tandika alipongeza uongozi wa Mfuko kwa kuandaa mafunzo haya kwa watumishi wapya. Pia alisema mafunzo haya ni muhImu kwa kuwa watumishi watafundishwa maadili kuhusu utumishi wa Umma ndio nguzo ya utendaji kazi, lakini mtumishi wa umma ni taswira ya serikali, hivyo ni muhimu kupata mafunzo kwa lengo la kuwezesha kila mmoja kujitambua na kutambua nafasi yake.
Mafunzo haya yatajumuisha mada mbalimbali zitakazotolewa na wakufunzi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma, ambazo ni Maadili ya Utumishi wa Umma na uwajibikaji, Muundo wa Serikali na Shughuli zake, Menejimenti ya Kumbukumbu na mawasiliano ya kiofisi, Misingi ya Sheria na kanuni za Utumishi wa Umma, Elimu ya Usalama wa Serikali na ujazaji wa fomu za maalum za kiutumishi na mada kuhusu shughuli za Mfuko kutoka katika Kurugenzi na Vitengo mbalimbali ili kujua namna Mfuko unavyofanya kazi.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unaendelea kutoa mafunzo elekezi kwa watumishi wake mara kwa mara ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi, weledi na kuendelea kuboresha huduma kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge sasa