NHIF TUMIENI FURSA GEITA- Mhe. Shigela

Imewekwa: 08 August, 2025
NHIF TUMIENI FURSA GEITA- Mhe. Shigela

Na Mwandishi Wetu, Geita

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umeombwa kutumia fursa za uwepo wa vyama vya wachimbaji madini mkoani Geita kwa lengo la kuongeza wigo wa wanachama hususan katika kipindi hiki cha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.

Rai hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela wakati akizungumza na Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF iliyoongozwa na Kaimu Mwenyekiti Dkt. Zubeda Chande.

Alisema kuwa Mkoa wa Geita unazo fursa nyingi kutokana na shughuli kubwa za kiuchumi zinazoendelea mkoani hapo ambazo zinawawezesha wananchi kumudu gharama za kujiunga na bima ya afya na kuwa na uhakika wa matibabu wakati wote.

“Hapa tunavyo vyama vya wachimbaji wadogo wadogo ambao wana uwezo wa kifedha kulipia gharama za kujiunga hivyo wekeni mikakati ili tushirikiane kwa pamoja kuwafikia na kuwapa elimu ya umuhimu wa kuwa ndani ya mfumo wa bima ya afya,” alisema Mhe. Shigela.

Alisema kuwa NHIF ni nguzo kubwa katika ustawi wa jamii hivyo ni wajibu kuhakikisha wananchi wanafikiwa na wanahamasishwa kujiunga na hatimaye kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha.

Katika hatua nyingine  alipongeza Mfuko kwa kazi kubwa inayofanya ya kuwahudumia watanzania na akaahidi ofisi yake iko tayari kushirikiana katika kutoa elimu lakini pia kusimamia huduma zinazotolewa na watoa huduma ili ziwe bora zaidi na kuvutia zaidi wananchi kujiunga na NHIF.
Kwa upande wake Dkt. Chande kwa niaba ya Bodi, alishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ushirikiano inaotoa kwa Mfuko, unaowezesha kuwafikia wananchi kwa urahisi hatimaye kuwezesha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.

“Tunafarijika sana kama Bodi tunapopata mrejesho kama huu kutoka kwenu viongozi, tunaamini hata utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote utakuwa wenye ufanisi zaidi na tutatimiza ndoto ya Serikali ya kila mwananchi kuwa na Bima ya Afya,” alisema Dkt. Chande.

Wajumbe wa Bodi na Mnejeimenti ya NHIF ikiongozwa na Bi. Zubeda Chande wakisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela walipomtembelea ofisini kwake wakiwa katika ziara ya kikazi katika Mkoa wa Geita.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa Mfuko uko tayari na umejipanga kuhudumia wananchi wengi zaidi ambapo umefanikiwa kufanya maboresho ya Mifumo inayowezesha kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa lakini pia maboresho katika huduma za matibabu ambazo zimezingatia mahitaji halisi na gharama nafuu.

“Tunashukuru sana kwa kutuonesha fursa zilizopo hapa, mimi na wenzangu tutalifanyia kazi kwa haraka kwa kuja kukutana na vyama hivi lakini pia Watoa huduma kuona mahitaji yao ya maboresho ili waweze kutumia fursa ya Mikopo ya Vifaa tiba, TEHAMA, dawa na ukarabati wa miundombinu na hii inasaidia kuboresha huduma kwa ajili ya wanachama wetu na wananchi kwa ujumla,” alisema Dkt. Isaka.

BIMA YA AFYA KWA WOTE, JIUNGE SASA