27/09/2025 Songwe
Mwenyekiti wa msafara wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Prof. George M. Ruhago, akiwa ziarani mkoani Songwe amewataka watumishi wa Ofisi ya NHIF Songwe kusimamia ubora wa uchakataji wa madai ya watoa huduma ili kupunguza malalamiko yanayotokana na makato kwenye madai yanayowasilishwa.
Amesema makato mengi yanaweza kuashiria udanganyifu au ukosefu wa uelewa wa taratibu kwa watoa Huduma.
Prof. Ruhago aliwapongeza kwa juhudi zao na kuwataka kuendelea kujipanga kuelekea utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, sambamba na kutumia rasilimali za Mfuko kwa uangalifu ili kuleta tija na manufaa kwa wanachama.
Aidha, Mjumbe wa Bodi CPA Dickson A. Kaambwa aliwasisitiza kuandaa mipango inayopimika ili wakati wa kufanya tathmini waweze kubaini changamoto zinazokwamisha kufikia malengo, huku akiipongeza ofisi kwa mafanikio ya usajili wa waajiri katika mkoa huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Irene C. Isaka, aliipongeza ofisi hiyo kwa kutokuwa na mashauri ya kinidhamu pamoja na ushirikiano mzuri NHIF na taasisi za serikali mkoani humo. Pia aliwataka kutumia wadau mbalimbali kama mabenki, viongozi wa kiimani na kimila pamoja na mawakala na vyama vya ushirika katika kufanikisha Bima ya Afya kwa Wote.
Dkt. Isaka vilebile aliwakumbusha kuhamasisha vituo vya Afya kuchukua mikopo ya vifaa tiba, dawa na majengo ili kuboresha huduma za Afya kwa wanachama.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa