NHIF Lindi yaanza utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kwa Kishindo!

Imewekwa: 10 December, 2025
NHIF Lindi yaanza utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kwa Kishindo!

NHIF Mkoa wa Lindi imekutana na waratibu wa Mfuko kutoka Halmashauri zilizopo mkoa wa Lindi pamoja na wawakilishi wa Hospitali za Rufaa kujadili namna bora ya kuboresha utekelezaji wa majukumu na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Kikao kazi kilichofanyika tarehe 5 Desemba 2025 kilijikita kwenye kuboresha uwasilishaji wa madai kupitia mifumo ya kidigitali, kuhakikisha usahihi wa uandaaji wa madai, kuwasilisha madai kwa wakati, kufuata miongozo ya NHIF ili kupunguza makato, na kuimarisha ushirikiano kati ya waratibu na wataalam wa hospitali katika uhakiki wa huduma.

Meneja wa NHIF Lindi, Bi. Janeth Kibambo, alitumia fursa hiyo kuwaeleza wadau kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote na kuwahimiza kuongeza uhamasishaji kwa wananchi pamoja na kuboresha mifumo ya utambuzi wa wanachama kwenye vituo vya huduma.

Washiriki wa kikao hicho, walitoa maoni na changamoto wanazokutana nazo, ambapo NHIF ilitoa ufafanuzi na kuahidi kuendelea kuboresha maeneo yaliyopendekezwa.

Kikao hiki kimeongeza uimara wa ushirikiano kati ya NHIF, Halmashauri na vituo vya kutolea huduma, huku wakikubaliana kuimarisha mawasiliano ya kila siku, kufanya ufuatiliaji wa ubora wa huduma, kukuza matumizi ya TEHAMA na kuendelea kujiandaa na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.

Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge sasa