Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umekuwa mshindi wa kwanza katika umahiri wa ufungaji wa Hesabu ya Taasisi za Bima kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2024.
Ushindi huo katika kundi (category) ya Sekta ya Bima ni kielelezo cha weredi, uwazi na uwajibikaji wa Mfuko katika kulinda rasilimali za wanachama na uendelevu wa Mfuko.
Akikabidhi tuzo hiyo, kwa Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF ambaye ni Mhasibu Mkuu wa Mfuko CPA. Happiness J. Sima, Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Laurent Deogratius Luswetula alipongeza Mfuko kwa kupata tuzo hiyo, inayodhihirisha kuwa Mfuko unazingatia Utawala Bora katika utekelezaji wa majukumu yake.
Tuzo hizo huandaliwa kila mwaka na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) kwa lengo la kutambua taasisi zinazozingatia miongozo na taratibu za kitaifa na kimataifa za uandaaji wa hesabu.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko Dkt. Irene C. Isaka alisema, anapokea tuzo hiyo kwa unyenyekevu mkubwa, huku akitoa salamu za pongezi toka Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko kwa watumishi wote kwa kufikia mafanikio hayo .
Dkt. Isaka alisisitiza kuwa, tuzo hiyo iwe chachu kwa Mfuko kuongeza juhudi zaidi ili kuongeza imani kwa wanachama na wadau kwa ujumla
Mahesabu ya Mfuko ni moja ya eneo linalouthibitishia umma namna Mfuko unavyowajibika kwa wadau wake kwa uwazi na kuzingatia misingi ya Utawala Bora, alisema Dkt. Isaka.
Aidha, Mkurugenzi wa Fedha CPA Grace Temba akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi tuzo hiyo kwa Menejimenti ya Mfuko, alisema kwamba mwanzoni mfuko ulikuwa ukitumia vigezo vya kufunga nahesabu kama vile vinavyotumiwa na mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Lakini sasa tunapoendelea na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, Mfuko unatumia migezo vya kibima yaani IFRS 17.
Naye CPA Mustafa alitoa shukrani kwa Mkurugenzi Mkuu na Menejimenti kwa kuweka mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na mafunzo ya mara kwa mara kwa kurugenzi ya Fedha na hivyo kuongeza weledi katika uandaaji wa hesabu za Mfuko.
Kwa mwaka huu hafla ya utoaji tuzo hizo ilifanyika jijini Dar es Salaam siku ya Disemba 4, 2025.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa