Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana na Ajira, Mhe. Kedmon Mapana, amepongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kuhamasisha Wasanii na kuwapatia elimu ya umuhimu wa kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, ili waweze kushiriki kikamilifu na kuwa mabalozi wa uhamasishaji kwa jamii.
Mhe. Mapana aliyasema hayo alipotembelea banda la NHIF wakati wa ufunguzi wa kongamano la Sanaa Pesa Festival linalowakutanisha zaidi ya vijana 3,000, lililofanyika katika viwanja vya EACLC, Ubungo jijini Dar es Salaam.
Alisisitiza kuwa kundi la wasanii lina mchango mkubwa katika kufikisha ujumbe kwa jamii, hivyo ni muhimu kupewa kipaumbele katika utoaji wa elimu kuhusu bima ya afya ili kusaidia kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika mpango huo.
“Wakati mnatekeleza bima ya afya kwa wote, hakikisheni kwenye mpango kazi wenu mnawafikia na kuwapa elimu wasanii waweze kujiunga kwa wingi, lakini pia kuwahusisha kwa karibu ili wawe mabalozi wazuri wa kuhamasisha jamii,” alisema Mhe. Mapana.
Aidha, aliipongeza NHIF kwa kushiriki katika maonesho hayo ya siku tatu, akieleza kuwa ushiriki huo unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuhakikisha mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unafanikiwa na kuchangia kuboresha huduma za afya nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Uanachama wa NHIF, Bw. Gwelino Wissa, alimueleza mgeni rasmi kuwa Mfuko Mfuko umeanza mawasiliano na viongozi wa vyama vya wasanii wa makundi mbalimbali kwa lengo la kufanya uhakiki wa wanachama wao mapema. Hatua hiyo inalenga kuweka msingi imara wa usajili wa wasanii watakapopewa kipaumbele katika utekelezaji wa mpango huo.
Maonesho ya Sanaa Pesa Festival pia yamewakutanisha wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za kifedha, mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na mashirika mengine, yakilenga kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii kupitia ubunifu na fursa mbalimbali.
Kwa ujumla, ushiriki wa NHIF katika kongamano hilo unaendelea kudhihirisha dhamira ya Mfuko katika kuwafikia makundi mbalimbali ya jamii, hususan vijana na wasanii, ili kuhakikisha lengo la kuwa na Bima ya Afya kwa Wote linafanikiwa nchini.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa