Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umetajwa kuwa ni Mfuko wenye mtandao mkubwa unaoweza kufanikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kuwafikia na kuwasajili wananchi kwenye mfumo wa bima ya afya.
Mtandao huo utatumika kufikisha elimu ya dhana ya bima ya afya, uhamasishaji wa wananchi na usajili wa wanachama wakati wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana wakati akizungumza na Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF ofisini kwake ambayo ilifika kwa lengo la kuweka mkakati wa kuwafikia wananchi na kupata mrejesho wa huduma kwa lengo la kuboresha zaidi.
Akizungumzia namna ya kuwafikia wananchi, aliutaka Mfuko kuangalia uwezekano wa kuwawezesha wananchi wote kujiunga kupitia vifurushi mbalimbali ili waweze kuchagua na kujiunga ili kuwa na uhakika wa huduma za matibabu wakati wanapozihitaji.
“Bima ya Afya kwa Wote ndio mkombozi wa wa wananchi katika kupata huduma za matibabu hivyo naamini kupitia mtandao wenu mkubwa hapa nchini mtaweza kuwafikia wananchi wote ili kutimiza lengo la Serikali la wananchi kupata huduma bora kupitia bima ya afya” alisema Bw. Elikana.
Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wakiongzwa na Bi. Zubeda Chande wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mfuko ofisi ya Mwanza wakiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo mapema wiki hii.
Alisema kuwa endapo wananchi watafikiwa na kujiunga itawasaidia kuwa na uhakika wa kupanga na kushiriki kikamilifu shughuli za maendeleo na hatimaye kukuza uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.
“Hakuna mbadala wa bima ya afya kwa kuwa ndio njia pekee inayomwezesha mwananchi kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu bila kikwazo chochote na kwa uwekezaji uliofanyika kwenye sekta ya afya umewezesha upatikanaji wa huduma bora na zenye uhakika,” alisema.
Akizungumzia mikakati ya kuwafikia wananchi, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Irene Isaka alisema kuwa Mfuko umejioanga katika maeneo yote kuhakikisha wananchi wanafikiwa na kusajiliwa.
“Tunaendelea na utoaji wa elimu na kuhamasisha wananchi kujiunga kupitia vifurushi mbalimbali lakini pia tumeendelea kuboresha uoatikanaji wanhuduma,” alisema Dkt. Isaka.
Akitoa salaam za Bodi Kaimu Mwenyekiti wa Bodi Dkt. Zubeda Chande alisema kuwa Mfuko utaendelea kushirikiana na Ofisi ya Serikali ya Mkoa katika kuwafikia wananchi na kutimiza ndoto ya Serikali.
Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa