Mkuu wa Mkoa wa Tanga Apongeza Mapinduzi kwenye Huduma za NHIF*

Imewekwa: 14 June, 2025
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Apongeza Mapinduzi kwenye Huduma za NHIF*

Mkuu wa mkoa wa Tanga Dkt.Balozi Batilda Salha Buriani amepongeza maboresho mbalimbali ya kihuduma yanayofanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa wanachama wake ikiwemo maboresho ya ulipaji wa madai kwa watoa huduma ambapo sasa yanalipwa kwa wakati na kupunguza malalamiko. 

Ameyasema hayo katika mkutano wa Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri ya Mji Handeni na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) uliofanyika Juni 12, 2025 mkoani Tanga. 

Mkuu wa Mkoa alisema “hapo nyuma kulikuwa na changamoto ya ucheleweshaji wa ulipaji wa madai kutoka NHIF ambapo ilisababisha kutokea hadi kwenye taarifa ya CAG lakini baada ya maboresho ya mifumo yaliyofanywa na NHIF sasa madai yanalipwa kwa wakati na kuondoa hoja’’.

Meneja wa NHIF Bw.Evance Nyangazi akiwasilisha mada ya maboresho ya huduma za Mfuko katika mkutano wa baraza la madiwani wa halmashauri ya mji Handeni na Halmashauri ya wilaya ya Handeni Mkoani Tanga mapema wiki hii.

Akizungumzia maboresho hayo Meneja wa Mfuko wa NHIF Mkoa wa Tanga Bw. Evance Nyangazi  amesema maboresho yaliyofanyika katika mfumo wa uchakataji na ulipaji wa madai umerahisha katika kuboresha eneo la ulipaji ambapo ofisi yake imeshalipa madai yote ya watoa huduma hadi  mwezi April 2025. 
Aidha amesema mafanikio haya yametokana na maboresho makubwa katika mifumo ya uwasilishaji wa madai kwa njia ya mtandao na amewasihi viongozi wa Halmashauri kusimamia kikamilifu suala la uwasilishaji wa madai kufanyika ndani ya saa 24 baada ya mzunguko wa huduma.

Wananchi na wakuu wa idara za halmashauri za Mji Handeni na Halmashauri ya wilaya ya Handeni wakifuatilia mkutano wa baraza la madiwani la taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za serikali.
Kwa upande wa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Bw. Nyangazi aliwaeleza Viongozi na Waheshimiwa madiwani  Mfuko unaendelea kutoa elimu ya umuhimu wa kila mtanzania kujiunga na huduma za bima ili kuwa na uhakika wa matibabu wakati wote.

Hata hivyo aliwaomba kutumia majukwaa mbalimbali kama Viongozi kupenyeza elimu hii kwa wananchi ili kila mwananchi aelewe umuhimu wa kujiunga na huduma za bima ya afya kabla ya kuugua.

Hata hivyo aliwahakikishia kwamba Mfuko umejizatiti katika kutoa huduma bora kwa wanachama wake na wanufaika wote wa Mfuko kwani sasa mwanachama anaweza kujihudumia mahali popote bila ya kufika ofisi kwa kutumia mfumo wa NHIF Jihudumie (Self Service)..