MKURUGENZI MKUU ATEMBELEA OFISI YA NHIF MKOA WA TANGA

Imewekwa: 21 October, 2025
MKURUGENZI MKUU ATEMBELEA OFISI YA NHIF MKOA WA TANGA

20 Oktoba, 2025                       Tanga

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Dkt. Irene C. lsaka amefanya ziara ya kikazi katika ofisi ya Mfuko Mkoa wa Tanga ikiwa ni sehemu ya kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa utendaji kazi wa Ofisi za Mikoa kuelekea utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote.

Akiwa katika ziara hiyo Mkurugenzi Mkuu amepokea taarifa ya utendaji ya Mkoa wa Tanga kwa robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2025/26  na kuridhishwa na utendaji kazi ulio bora wa Ofisi hiyo. 

Mkurugenzi Mkuu ameridhishwa na kasi ya uchakataji na ulipaji wa madai ya watoa huduma kwa wakati, ambapo kwa sasa kasi ya ulipaji ni wastani wa siku 30 ukilinganisha na wastani wa siku 72 kwa kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2024/25.

Dkt. Isaka amepongeza mikakati iliyoweka na Ofisi ya Mkoa katika kuongeza kasi ya usajili kwa kuyafikia makundi mbalimbali ya wananchi kama Wanafunzi, Vyama vya Ushirika na AMCOS ambapo katika kipindi cha robo ya kwanza Ofisi imefanikiwa kuwafikia  wanachama wa Ushirika wapatao 8,466.

Na katika Upande Mwingine Mkurugenzi Mkuu amesema kuwa ili kufanikisha usajili wa makundi hayo, Menejimenti imeridhia kuwepo kwa kifurushi maalum kwa ajili ya Vyama vya Ushirika katika  kuelekea utekezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, ikiwa ni jitihada za kutambua mchango wa wakulima kama uti wa mgongo wa uchumi wa Nchi.

Ili kuendelea kulinda mitaji ya wajasiriamali na wafanyabiashara wadogowadogo, Dkt. Isaka ameelekeza Ofisi ya Mikoa kuendeleza mashirikiano na taasisi za kifedha na Benki zinazotoa mikopo kwa wafanyabiashara kuona namna bora ya kuwakatia bima ya afya wateja wao kwa kuweka utaratibu wa marejesho kidogo kidogo, na tayari taasisi mbalimbali za kifedha  zimeonesha utayari wa kufanya kazi na Mfuko katika kutoa huduma kwa kundi hilo.

hata hivyo, ameitaka ofisi ya Mkoa kutumia fursa ya kuendelea kutoa elimu ya Bima ya Afya kwa uongozi wa vyama vya wafanyabiashara, pamoja na kutembelea nyumba za Ibada.Lkini pia alitumia wasaa huo kuwataka watumishi kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi pamoja na kutoa huduma bora kwa wateja hasa wakati huu tunapoelekea katika utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.

Mwisho, watumishi wa Mkoa wa Tanga walimuahidi Mkurugenzi Mkuu kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha lengo la Taasisi na matarajio ya Serikali ya uwepo wa uhakika wa Bima ya Afya kwa wote.

Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa