MHE. JENISTA MHAGAMA AZINDUA BODI YA NHIF

Imewekwa: 21 January, 2025
MHE. JENISTA MHAGAMA AZINDUA BODI YA NHIF

Waziri wa Afya Mhe. Jenister Mhagama amezindua Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ambapo ameitaka kuwafikiria wananchi wa kawaida kwenye kila maamuzi wanayofanya hususan ya kuwawezesha kupata huduma za matibabu kupitia mfumo wa bima ya afya.

Uzinduzi huo umefanyika jana Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo Bunge, wadau wa sekta ya afya, wanahabari na wadau wa bima nchini.

Mhe. Waziri ameitaka bodi hiyo kuhakikisha inasimamia vyema suala la utekelezaji wa bima ya afya kwa wote na kufanya kazi kwa karibu na sekta binafsi ili kufanikisha utoaji wa huduma bora kwa wanachama.

“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yeye amemaliza kazi yake ya kuwekeza katika huduma za matibabu kazi yenu sasa ni kuwezesha wananchi kutumia huduma hizo kupitia bima ya afya hivyo ni matarajio yangu kuwa bodi hii mbakwenda kusimamia haya kwa nguvu zote” alisema Mhe. Waziri.

Bodi iliyozinduliwa inaongozwa na Bw. Eliud Sanga ambaye ni Mwenyekiti akiwa na wajumbe wake wanane wenye uzoefu mbalimbali katika masuala ya afya na bima kwa ujumla.