Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Apongeza Uboreshwaji wa Huduma za NHIF

Imewekwa: 13 June, 2025
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Apongeza Uboreshwaji wa Huduma za NHIF

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Razack Lokina, amesifia mafanikio ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika kuboresha na kurahisisha huduma zao kupitia mifumo ya kidijitali na mtandaoni.  

Alisema hayo wakati akizungumza katika zoezi la utoaji wa huduma za matibabu bure kwa wananchi wa Hombolo kuelekea kongamano la afya lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma, katika Kata ya Hombolo, Jijini Dodoma, ambapo NHIF ilishiriki kama mshiriki na mdhamini.  

Profesa Lokina alibainisha kuwa mabadiliko ya kiteknolojia yanayotekelezwa na NHIF yamepunguza changamoto za wanachama na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wateja. 

Meneja Masoko wa Mfuko  wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bi. Anjela Mziray akitoa maelezo ya maboresho ya kihuduma  kwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wakati alipotembelea banda la NHIF katika kuelekea kongamano la Afya linalofanyika katika viwanja vya Hombolo jijini Dodoma.

Kwa upande wake, Meneja wa Masoko na Huduma kwa Wateja wa NHIF, Bi. Anjela Mziray, alieleza jinsi mifumo hii mpya inavyowasaidia wanachama kwa kuwapunguzia usumbufu na kuwawezesha kupata huduma kwa urahisi zaidi. "Tumekuwa na mabadiliko makubwa katika mfumo wetu, hasa kwa kutumia teknolojia, ambayo inahakikisha huduma zinawafikia wanachama haraka na kwa ufanisi," alisema Bi. Mziray.  

Aidha, Profesa Lokina alipongeza juhudi za NHIF katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa bima ya afya katika maeneo mbalimbali nchini. "Hatua hizi za uhamasishaji na uboreshaji wa huduma zinaongeza imani ya wananchi katika mfumo wa afya wa nchi yetu," aliongeza.  

Elimu ya Mfumo wa NHIF Self Services ikiendelea kutolewa kwa wananchi wanaotembelea banda la NHIF katika Kongamano la Afya lililoandaliwa na Chuo kikuu cha Dodoma.

Kongamano hilo linalenga kujadili mambo mbalimbali yanayohusu afya, ikiwemo ubora wa huduma, teknolojia katika sekta ya afya, na mifumo ya bima kwenye upatikanaji wa matibabu kwa wananchi wote.