Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umepokea ujumbe kutoka Jamhuri ya Shirikisho la kidemokrasia ya Ethiopia uliowasili nchini kwa lengo kujifunza kuhusu huduma za bima ya afya.
Ziara hiyo ya mafunzo imelenga kuwajengea uwezo wataalamu wa Ethiopia kwa kujifunza mbinu na mifumo mbalimbali inayotumiwa na NHIF kutoa huduma bora za bima ya afya.
Ujumbe huo uliongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu, Huduma ya Bina ya Afya ya Ethiopia Yametot Andualem, umepata fursa ya kujifunza maeneo mbalimbali ya uendeshaji wa Mfuko, ikiwemo : utambuzi, usajili, ukusanyaji michango, uchakataji madai, ulipaji na udhibiti wa udanganyifu kwa kutumia mifumo. Vile vile walijifunza kuhusu utoaji wa huduma za bima ya afya, uratibu wa kisekta na ushirikiano wa wadau mbalimbali, pamoja na mikakati inayotumika kuhakikisha Mfuko unaendelea kuwa imara na endelevu kifedha.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu NHIF - Dkt Rose Ntundu aliwaelezea wageni hao namna NHIF inavyotekeleza programu za elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima ya afya, taratibu za usajili wa vituo vya kutolea huduma za afya, mifumo ya malipo kwa watoa huduma, pamoja na mbinu za kisasa za udhibiti wa ubora wa huduma na kudhibiti udanganyifu katika matumizi ya bima ya afya.
Kupitia ziara hiyo ya mafunzo, ujumbe wa Ethiopia umefanikiwa kujionea kwa karibu namna NHIF ilivyojenga mifumo madhubuti inayowezesha utoaji wa huduma kwa wanachama kwa ufanisi huku ikihakikisha matumizi sahihi ya rasilimali na kuongeza imani ya wananchi kwa mfumo wa bima ya afya.
Kwa miaka ya hivi karibuni, NHIF imevutia nchi mbalimbali kuja kujifunza kuhusu uendeshaji wa bima ya afya kwa wote.
Kutokana na mafanikio hayo, Mfuko umekuwa ukipokea wageni kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika na nje ya bara hilo wanaofika kujifunza uzoefu wa Tanzania katika kuendesha mifumo ya bima ya afya.