Bodi ya Wakurugenzi NHIF Yatembelea Ruvuma

Imewekwa: 26 June, 2025
Bodi ya Wakurugenzi NHIF Yatembelea Ruvuma

Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF Bw. Eliud Sanga akiambatana na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF Dkt. George Ruhago na Dkt. Zubeda Chande pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Irene Isaka amefanya ziara ya kikazi mkoani Ruvuma na kujionea hali ya utoaji wa huduma za NHIF katika Mkoa huo na kuzungumza na Watumishi.

Pamoja na azma hiyo, pia Mwenyekiti wa Bodi alitembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na kukutana na Mkuu wa Mkoa Kanali Ahmed Abbas Ahmed na kuzungumza mambo kadhaa kuhusu uboreshaji wa huduma za Bima ya Afya katika Mkoa huo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi alibainisha kuwa NHIF itajenga ofisi yake katika Mkoa huo na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za bima ya afya kwa wananchi na jengo hilo litakuwa kitega uchumi kitakachoongeza mapato ya Mfuko.

Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa  NHIF ofisi ya Ruvuma wakati wa ziara ya kikazi mkoani humo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa Kanali Ahmed alitoa wito kwa NHIF kuendelea kuwekeza katika miradi ambayo ni vitega uchumi itakaya sukuma maendeleo ya mkoa huo na kuahidi kutoa ushirikiano wote utakaohitajika na NHIF.

Mjumbe wa Bodi, Dkt. Zubeda, alitoa rai kwa Mkuu wa Mkoa kuendelea kuhimiza wananchi kujiunga na mfumo wa bima ya afya kwa ulinzi wa afya zao na kuepusha matumizi ya fedha nyingi katika matibabu. 

Naye Mjumbe wa Bodi Dkt. George, aliwataka Ofisi ya Mkoa kuendelea kufanya uchambuzi wa malipo ya madai na kuhakikisha yanafuata taratibu na kanuni zilizowekwa ili kuepusha upotevu wa fedha. 

Mkurugenzi Mkuu Bi. Irene Isaka alishukuru kwa Bodi kutenga muda kwa ajili ya kujionea yanayoendelea katika ofisi za Mikoa na kutoa rai kwa watumishi kuendelea kujituma katika usajili wa wanachama na kufikia azma ya Serikali ya Bima ya Afya kwa Wote.

Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa