Na Mwandishi Wetu, Mara
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evance Mtambi amesema kuwa kuanza utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kutasaidia kuondoa changamoto za huduma za matibabu kwa makundi yote ya wananchi.
Kutokana na hilo ameutaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuendelea kuimarisha Mifumo yake ikiwemo ya utambuzi na udhibiti wa vitendo vyenye viashiria vya udanganyifu ili uhai na uhimilivu wa Mfuko uendelee kuimarika.
Haya ameyasema jana ofisini kwake wakati akizungumza na Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF iliyofika ofisini hapo kwa lengo la kuweka mikakati ya ushirikiano katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ili wananchi waweze kujiunga na kuwa na uhakika wa huduma za matibabu wakati wote.
“Uwepo wa Bima ya Afya kwa Wote utasaidia makundi yote yakiwemo ya Wazee, watoto, walemavu na makundi mengine kunufaika na huduma za matibabu kupitia mfumo wa bima ya afya,” alisema Mhe. Kanali Mtambi.
Kutokana na hayo alitoa rai kwa NHIF kuongeza wigo wa utoaji wa elimu kwa wananchi hususan wa maeneo ya vijijini ili wafahamu umuhimu wake na wachukue hatua ya kujiunga.
Kwa upande wa Ofisi ya Mkoa, aliuhakikishia Mfuko ushirikiano katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ili lengo la kila mwananchi kuwa ndani ya mfumo wa bima ya afya litimie.
Mkurugenzi mkuu Dkt.Irene Isaka akizungumza na watumishi akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mara.
Akizungumzia utayari wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Irene Isaka alisema maandalizi makubwa yaliyofanywa ni pamoja na maboresho ya mifumo ambayo inasomana na taasisi zingine kwa ajili ya kupata taarifa za wanachama kwa haraka.
“Mifumo yetu kwa sasa inasomana na inatuwezesha kupata taarifa za mwanachama wakati anapopata huduma hospitali na inasaidia kwa kiwango kikubwa kudhibiti vitendo vya udanganyifu” alisema Dkt. Isaka.
Kwa upande wa Bodi ya Wakurugenzi iliyoongozwa na Dkt. Zubeda Chande alisema Mfuko utaendelea na uboreshaji wa huduma kwa kuzingatia uhai na uhimilivu wa Mfuko ili uendelee kuwa imara na kutoa huduma bora.
Alisema kuwa mrejesho unaopatikana kupitia wanachama, wananchi na viongozi wa serikali unasaidia katika kufanya maboresho na kutatua changamoto zinazohitokeza katika huduma.
“Tunashukuru sana kwa ushirikiano ambao mnatupatia kupitia Ofisi yako ili kufanikisha utekelezaji wa shughuli zetu, kazi kubwa iliyoko mbele yetu ni kuwafikia wananchi na wajiunge ili wapate huduma wanapozitaka,” alisema Dkt. Chande.
Bima ya Afya kWa Wote, Jiunge sasa