Na Mwandishi Wetu, Geita
Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), imeiagiza Ofisi ya Mkoa wa Geita kutumia fursa zilizopo mkoani humo kuwahamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu.
Agizo hilo lilitolewa jana na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dkt. Zubeda Chande wakati akizungumza na Watumishi wa NHIF Mkoa wa Geita muda mfupi baada ya kuwa na kikao na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Martin Shigela.
Alisema kuwa Mkoa wa Gaita unazo fursa nyingi kutokana na uwepo wa shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uchimbaji wa madini, uvuvi, Kilimo na biashara. Shughuli ambazo zinawezesha wananchi kuwa na kipato cha kugharamia mahitaji ikiwemo bima ya afya.
“Tumetoka kukutana na Mkuu wa Mkoa, ametueleza namna Mkoa ulivyo na fursa nyingi ikiwemo wananchi wake kuwa na uwezo wa kugharamia bima ya afya, nawaagiza kuweka mikakati yenu vizuri ili kuwafikia wananchi hawa kwa makundi. Nahimiza huduma bora kwa wanachama. Muweke usimamizi mzuri wa vituo tulivyovisajili ili tuweze kuvutia wananchi wengi na kuondokana na malalamiko” alisema Dkt. Chande.
Naye Mjumbe wa Bodi Wakili. Shaban Kabunga aliwataka Watumishi kuwa na malengo mahsusi yanayoweza kuleta matokeo katika usajili wa wanachama na ukusanyaji wa michango. Aliwataka kutumia takwimu kubainisha wadau na fursa zilizopo ili kuwezesha usajili wa wananchi.
Wajumbe wa Bodi wakutana na watumishi wa Mfuko Mkoa wa Geita
Naye Bw. Amour Amour ambaye ni Mjumbe wa Bodi na Mkurugenzi wa Mipango Wizara ya Afya, aliwataka Watumishi kuhakikisha wanasimamia ubora wa huduma zinazotolewa kwa wanachama na Vituo vya kutolea huduma ili kuwezesha kuvutia wananchi wengine kujiunga na bima ya afya. Alisema Sera ya Afya imejikita kwenye uboreshaji wa huduma za Afya hivyo kupitia Sera pamoja na Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ni fursa nzuri kwa NHIF kuongeza wigo wa wanachama.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka alisisitiza utendaji kazi unaozingatia maadili ya utumishi wa umma, ubunifu pamoja na kufuata Sheria, Kanuni, taratibu na miongozo iliyopo ili kuepukana na malalamiko na kuongeza ufanisi.
Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha Watumishi hao kuhamasisha vituo vya Afya kuhusu uwepo wa fursa za Mikopo ya vifaa tiba, dawa na ukarabati wa majengo unaolenga kuboresha huduma katika vituo vilivyosajiliwa na Mfuko.
“Tuvipitie vituo vyetu na kuangalia maeneo wanayoweza kuboresha kupitia mikopo yetu nafuu ili kuwezesha kutoa huduma bora zaidi kwa wanachama na wananchi kwa ujumla,” alisema Dkt. Isaka.
Naye Meneja wa Mkoa wa Geita Bw. Odhiambo, aliihakikishia Bodi kutekeleza maagizo ya Bodi ikiwemo kukutana na vyama vya wachimbaji wadogo wadogo wa madini ambao wana uwezo mkubwa wa kifedha wa kulipia bima ya afya.
BIMA YA AFYA KWA WOTE, JIUNGE SASA