NHIF YAPONGEZWA KWA KUJIIMARISHA KUELEKEA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Imewekwa: 25 July, 2025
NHIF YAPONGEZWA KWA KUJIIMARISHA KUELEKEA BIMA YA AFYA KWA WOTE

24 Julai, 2024-Arusha
 
Naibu waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus C. Sangu ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuendelea kuimarisha mifumo yake hasa tunapoelekea katika utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa Wote ambapo Mfuko ndio umepewa dhamana kubwa ya utekelezaji wa sheria hiyo.

Pongezi hizo ametoa alipotembelea banda la NHIF katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa Maafisa  Rasilimali Watu na Utawala (TAPA-HR) unaofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa  kituo cha kimataifa cha AICC jijini Arusha. 

Aliendelea kusema kuwa ni muda sahihi wa Mfuko kuendelea kujidhatiti na kuwa tayari katika maeneo ya teknolojia na kuhakikisha utoshelevu wa Watumishi ili kuhakikisha wakati wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote wananchi wanahudumiwa kwa ujumla wao bila changamoto yoyote.

Naibu Waziri Nchi- Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus C. Sangu akipata maelezo ya maboresho za huduma za Mfuko alipotembelea banda la NHIF katika Mkutano wa kwanza wa mwaka wa TAPA-HR uliofanyika jijini Arusha katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha AICC.

“Niwapongeze sana NHIF mlikua mnapitia changamoto nyingi sana ikiwemo watoa huduma kuwasilisha madai yasiyo na uhalisia, lakini sasa naona kutokana na maboresho ya mfumo wa uchakataji wa madai mmepunguza changamoto hiyo kwa kiasi kikubwa, alisema Mhe. Sangu.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Huduma za Uanachama wa NHIF Dkt. Alphonce Chandika alisema Mfuko umefanikiwa kutoa elimu ya maboresho ya huduma zake hasa katika Mfumo wa Usajili wa Wanachama kupitia Mfumo wa NHIF Jihufumie (Self Service) kwa washiriki wa Mkutano huu ambao ni wadau wakubwa katika usimamizi wa Rasilimali Watu katika taasisi zao.

Aidha Mfuko umeboresha huduma zake ikiwemo kuanzisha vifurushi mbalimbali ili kuwezesha wananchi kujiunga na huduma za Mfuko na kuwa na uhakika wa matibabu hasa tunapoelekea katika utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa Wote.

Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge sasa